24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kampeni ya kuongeza tija pamba yazinduliwa

Na Derick Milton, Busega

Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imezindua rasmi kampeni mpya inayolenga kuongeza tija katika zao la pamba nchini, ambapo lengo kuu ni kuongeza uzalishaji kutoka kilo 200 za pamba katika hekari moja hadi kilo 1,000.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Jumapili Julai 4, 2021 na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda katika kijiji cha Kijereshi kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na viongozi wote wa mkoa huo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga, amesema kuwa katika zao la pamba tatizo kubwa limekuwa siyo bei ya zao hilo kama ambavyo wakulima wanasema bali tatizo ni tija.

Mtunga amesema kuwa wakulima wengi nchini wamekuwa wakitumia nguvu katika kuzalisha badala ya kutumia maarifa, ambapo wengi wao wanashindwa kutumia maarifa mengi na wanatumia nguvu.

Amesema kuwa bodi ya pamba kupitia mkakati huo imejipanga kuhakikisha inabadilisha mfumo wa uendeshaji kilimo hicho kwa wakulima, ambapo katika msimu ujao wa pamba lengo ni kufikia uzalishaji wa tani 300,000 kutoka tani 122,000 msimu wa mwaka huu.

“Kwa wakulima wetu tatizo siyo nguvu, tatizo ni maarifa kwenye uzalishaji, ikiwa tutaweza kuongeza tija kwenye zao la pamba, hakuna mkulima ambaye atakuja hapa kulalamikia bei ya pamba, wakulima wetu wanazalisha kilo 175 hadi 250 kwa hekari moja, tunataka kufikia kilo 1,000,” amesema Mtunga.

Kaimu Mkurugenzi wa TARI Ukiruguru, Ereniko Kilembeka amewataka wakulima kutumia mbinu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na kituo hicho cha Ukiruguru baada ya kuzifanyia utafiti ili kuweza kunufaika na kilimo.

Amesema kuwa katika mkakati huo TARI Ukiruguru imekuja na mbinu mpya ya uzalishaji wa zao hilo kwa kiwango kikubwa, ambayo ni upandaji wa vipimo vya sentimeta 60 kwa 30 ambayo alisema ndiyo itatumiwa na wakulima katika kuongeza uzalishaji.

“Mbinu hii mpya ya upandaji kwanza inaongeza mazao shambani kwani hekari moja inakuwa na miche ya pamba 44,444, na mkulima akiweza kufuata kanuni bora za kilimo kwa kuweka samadi, kupulizia dawa kwa wakati atavuna kilo 1,000 hadi 1,400 kwa hekari moja,” amesema Kilembeka.

Naye Mtaalumu wa kilimo cha pamba kutoka Ukiruguru Dkt. Paul Saidia amemweleza Waziri kuwa baadhi ya wakulima katika mikoa ya Mwanza Mara, Shinyanga na Simiyu wameanza kutumia mbinu hiyo mpya ya upandaji kwa vipimo na kuona manufaa yake.

“ Kwa mbinu hii mpya ikiwa mkulima akiweza kulea vitumba 10 tu, kwa kuweka samadi, kupulizia dawa atapata kilo 1,400 kwa hekari moja, ikiwa atalea vituma 20 atapata kilo 2800 na hayo yatakuwa mapinduzi makubwa,” amesema Dkt Saidia.

Akizungumza mara baada ya kuzindua kampeini hiyo Waziri Mkenda, amesema kuwa serikali imejipanga katika eneo la tija ambapo imeongeza bajeti kutoka Milioni 603 hadi Bilioni 11.5

Waziri amesema kuwa eneo la kuongeza tija, limepewa kipaumbele ambapo amesema maafisa ugani wote nchini hasa kwenye zao la pamba watawezeshwa vifaa mbalimbali ili kuweza kuwafikia wakulima wote na kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles