Kampeni ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ yajaza damu Moi

0
719
Afisa Habari wa Taasisi ya Chakula na Lishe Jackson Monela na wananchi wengine wakichangia damu katika zoezi linaloendelea katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jana.

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM 

KAMPENI ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ imeongeza hamasa kwa wananchi na wadau kujitokeza kuchangia damu Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) ambayo jana imeweza kukusanya chupa zaidi ya 150.

Katika kampeni hiyo, wiki iliyopita wadau wa Asasi ya Family Federation for World Peace (FFWP) walichangia damu chupa 1,000.

“Tupo katika kampeni ya Tumeboresha Sekta ya Afya. Tuliweza kutumia nafasi hii kuhamasisha wananchi wajitokeze kuchangia damu hapa Moi na mwitikio umekuwa mkubwa na tunapata damu kuanzia chupa zaidi ya 100 kwa siku na hii ni faraja kubwa sana kwetu,” alisema Ofisa Habari  na Mahusiano  Moi, Patrick Mvungi.

Alisema FFWP imepeleka wananchi 1,500 kuchangia damu ambapo siku ya kwanza walikuwa 1,000 na siku ya pili 500 na wanatarajia kupokea wengine 500.

Aidha Mvungi alisema upatikanaji huo wa damu kwa sasa hakuna mgonjwa anayekosa kufanyiwa upasuaji kwani kuna damu ya kutosha. 

“Mahitaji ya damu Moi kwa siku ni chupa 15 hadi 30. Kabla ya zoezi hili la kuchangia damu, kwa siku tulikuwa tunapata chupa chini ya 15 na zilikuwa zinatoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama na wananchi wachache waliokuwa wanakuja kujitolea.

Kampeni ya Tumeboresha Sekta ya Afya inaendeshwa na maofisa habari kutoka Wizara ya Afya na taasisi zake ambayo itakuwa endelevu na Watanzania wanahamasishwa kujitokeza kuchangia damu kwa wenye mahitaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here