Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Charles Kichere, amesema mamlaka hiyo ina upungufu wa rasilimali watu 1,930 hali inayosababisha ucheleweshwaji wa ukusanyaji kodi na kutofungua ofisi zao katika baadhi ya wilaya na kuifanya serikali kukosa mapato ya maeneo hayo.
Kichere ameyasema hayo leo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya TRA katika kikao cha Rais Dk John Magufuli na mamlaka hiyo na wakuu wa mikoa kilichofanyika leo Jumatatu Desemba 10, jijini Dar es Salaam ambapo amesema mbali na upungufu huo pia wanahitaji nyumba 114 za wafanyakazi wa mipakani na ukarabati wa majengo 76 ya ofisi zao ili kuwapa mazingira mazuri ya kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuongeza mapato.
Aidha, Kamishna Kichere pia ameiomba serikali kupitia upya mfumo wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wadogo ili kuwasaidia kulipa kodi kwa hiari na kuwaandalia maeneo maalumu ya kufanyia biashara ili kuisaidia TRA kukusanya kodi kirahisi.
“Mahakama ya kodi ina kesi 50 zenye thamani ya Sh trilioni 25 ambazo hazijaamuliwa, tunaomba taratibu za kisheria ziharakishwe ili kesi hizi zitolewe maamuzi,” amesema Kichere.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema wizara yake kwa kushirikiana na TRA wataendelea kusimamia misingi bora ya ukusanywaji kodi, kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija na kupunguza tozo katika uanzishwaji wa biashara.
“Ili kuongeza ukusanywaji wa kodi kuna maeneo muhimu tutayazingatia kama kufanya ukaguzi bandarini, uwanja wa ndege na mipakani, kusimamia matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na ufuatiliaji wa mapato kutoka tasisi na mamlaka za serikali,“ amesema Waziri huyo.