24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

Kamishna Mkuu TRA azungumza na viongozi wa Wafanyabiashara Kasulu

Mwandishi Wetu -Kasulu

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata amezungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na Kigoma ambapo amesema timu ya wataalamu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka makao makuu itakaa mkoani humo wiki nzima ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

Katika ziara hiyo, Kidata ameambatana na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka TRA Makao Makuu akiwemo Kamishna wa Kodi za Ndani, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Naibu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa pamoja na timu ya watalaam wa kutoa elimu na huduma kwa mlipakodi.

Lengo la ziara hiyo ni ili kutatua changamoto zilizojitokeza wilayani humo na kuhakikisha wanapita kila duka yaani mlango kwa mlango kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu sheria na taratibu za ulipaji kodi.

Akizungumza na viongozi hao wa wafanyabishara katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kidata amesema kuwa, timu hiyo ya watalaam wa elimu kwa mlipakodi watakaa wilayani humo kwa wiki nzima wakipita duka kwa duka wakitoa elimu ya kodi na kutatua haraka changamoto za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara hususani makadirio ya kodi.

Amesema amepokea maoni, ushauri na changamoto zao na kwa kulitambua hilo amekwenda na timu ya watalaam kutoka TRA Makao Makuu ambao atawaacha mkoani hapo kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu sheria na taratibu za ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wao.

Amesema, pia watamsikiliza kila mfanyabiashara mwenye changamoto na kuzitatua.

“Ni muhimu kila upande yaani wafanyabiashara na watumishi wa TRA kuzingatia haki na wajibu wao kila wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Sisi watumishi wa TRA tunafanya kazi kwa kufuata misingi yetu ya maadili ambayo ni uwajibikaji, uadilifu na weledi lakini pia kama mmoja wenu alivyosema, ni lazima pia sote, ninyi na sisi TRA tuzingatie haki na wajibu kila tunapotekeleza majukumu yetu,” amesema Kidata.

Naye Prosper Guga ambaye ni Katibu wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Kasulu aliyezungumza kwa niaba ya viongozi wenzake amesema kuwa wamefurahishwa na kitendo cha Kamishna Mkuu wa TRA kufika wilayani hapo na kufanya nao mazungumzo pamoja na kupeleka timu ya watalaam kwaajili ya kuwapa elimu kwa walipakodi hao ikiwa ni pamoja na lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza baina ya wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na watumishi wa TRA.

“Ndugu Kamishna Mkuu, tunakushukuru sana kwa kuja kuzungumza na sisi na tumefurahi sana kwa kutuletea watalaam wa kutuelimisha na kutatua changamoto za mfanyabiashara mmoja mmoja kama zilivyowasilishwa kwako leo,” amesema Guga.

Aidha, kabla ya kuzungumza na viongozi hao wa wafanyabiashara wa Kasulu, Kidata aliwatembelea baadhi ya viongozi wa serikali mkoani humo ambapo alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu.

Pia, Kidata alizungumza na watumishi wa TRA wa Mkoa wa Kigoma na kuwataka kuzingatia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati na hiari huku wakiwapatia elimu ya kodi.

Hivi karibuni, wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walifanya mgomo na kufunga maduka wakidai kuwa watumishi wa TRA wilayani humo kutokuwa na lugha nzuri pamoja na kuwakadiria makadirio makubwa jambo lililopelekea kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, kutokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi mbalimbali wa serikali na wafanyabiashara hao, tayari maduka yamefunguliwa na shughuli za kibiashara zinaendelea kama kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,264FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles