24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 6, 2022

KAMISHNA MAGEREZA ALIYETIMULIWA KIKAONI NA LUGOLA ASTAAFU

NA GABRIEL MUSHI


ALIYEKUWA Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk. Juma Alli Malewa, amestaafu ikiwa ni wiki moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kumtimua kikaoni.

Julai 6, 2018, Lugola alimfukuza kikaoni Malewa kwa kosa la kuchelewa katika kikao cha kimkakati cha viongozi wa taasisi za wizara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Dk. John Magufuli, amemteua Naibu Kamishna wa Magereza, Phaustine Kasike, kuwa Kamishna Jenerali wa 14 wa Magereza kuanzia Julai 13, mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisema Kasike amechukuwa nafasi ya Malewa ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo, Kasike, alikuwa Mkuu wa Chuo cha Urekebishaji Tanzania (TCTA) Ukonga, Dar es Salaam.

Itakumbukwa kuwa Julai 6, 2018, Lugola alimfukuza kikaoni Malewa kwa kosa la kuchelewa kikaoni na kuagiza mlango kufungwa saa tano kamili asubuhi wakati kikao hicho kinaanza.

Hata hivyo, saa 5:01 asubuhi Malewa aliingia na ndipo Lugola alimwambia atoke nje na kuhoji kwanini amefunguliwa mlango.

Licha ya Malewa kuomba msamaha, Lugola alikataa kata kata na baada ya kuzungumza na wanahabari, Malewa na maofisa wengine waliruhusiwa kuingia ndani ya kikao.

Dk. Malewa ametumikia nafasi hiyo katika kipindi kifupi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 chini ya uongozi wa Magufuli.

Dk. Malewa aliteuliwa baada ya Magufuli kukubali na kuridhia ombi la kusitisha mkataba na kustaafu kwa Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna (CGP), John Minja.

Kutokana na ombi hilo, Dk. Magufuli alimteua Malewa kuwa Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini na baadaye kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Magufuli kufanya ziara katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam ambako alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini na watu binafsi na kutaka wote wanaofanya biashara hiyo kukabidhi kwa majeshi husika mara moja.

Alipiga marufuku hiyo kutokana na maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi kinyume na taratibu za majeshi nchini.

Pia alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,859FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles