Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digitala
KAMISHNA wa Utawala na Raslimali watu wa Jeshi la Polisi nchini, C.P Suzan Kaganda amewataka vijana hasa wasichana ambao ni wahitimu wa kidato cha sita kuwa na ndoto kubwa na mipango madhubuti ya kuweza kuzitimza ndoto hizo.
C.P Kaganda aliyasema hayo jana wakati wa mahafali ya 17 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansson kampasi ya Luguruni jijini Dar es Salaam.
Kaganda alisema ni muhimu kwa wasichana nchini kuwa na ndoto kubwa ambazo zinapimika na zinaweza kutekelezeka kwa wakati na muda sahihi huku wakizingatia maadili na kuwa chachu ya mabadiliko yaliyomema yenye kuzingatia utu na usawa.
“Kuweni na ndoto ambazo matokeo yake yanapimika na kutekelezeka, daima nawaombea kwa Mungu ili muweze kuwa na mafanikio makubwa ya kuweza kuzifikia ndoto zenu, kwa kuzingatia upendo na mshikamano iIi kuweza kuyabadili yale magumu kuwa mepesi.
“Mkumbute tu ukitaka kufika haraka nenda peke yako ila ukitaka kufika mbali nendeni kama team yaani pamoja, mkiwa na upendo na mshikamano wa kweli itawasaidia kufika mbali zaidi kwa pamoja na kupata mafanikio,” alisema Kaganda
Aidha aliwataka wasichana hao kuwa makini na utadawazi kwani unaweza kuwa na athari katika malezi na ukuaji wao na kwamba wanapaswa pia kuwa wakweli wa nafsi zao kwa kusimamia mambo wanayoyaamini maishani bila kuvunja sheria za nchi, shule na za nyumbani ambazo wazazi wameziweka.
“Kutokana na utandawazi wapo wengine utawaheshimu lakini wanaweza kukuvunjia heshima yako hivyo wasichana mnapaswa kuwa makini na wadadisi wa mambo na muwe na kiasi katika kupima na kutoa heshima hiyo, msitoe heshima kwa mtu ambaye hawaheshimu ili msije kuingia katika mitengo ya kidunia,” alisema
Aidha alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa elimu haina mwisho hivyo wasiache kujifunza na kuchukue ujuzi, maadili, mila, desturi, uvumilivu na uthubuti waliojifunza kutumia katika kuleta mabadiliko chanja kwenye jamii.
Kuhusu chagamoto inayoikabili shule hiyo ya upatikanaji wa fedha za kufadhili wasichana ambao familia zao zinakipato kidogo, alisema amewataka watu wenye uchungu na elimu kujitokeza katika kuwachagia wanafunzi wenye sifa kupata elimu katika shule hiyo.
“Jukumu la kusaidia elimu ni letu sote kama jamii, sisi tutaangalia litakalowezekana ili kuweza kusaidia ila tunawaomba watu wengine kujitokeza kusaidia kundi hili, pia nafahamu juu ya changamoto ya ardhi ya shule kuvamiwa na waarifu, niwaombe viongozi wa serikali mliopo hapa kuitafutia suluhisho la kudumu jambo hili,” alisema
Aidha Kaganda aliishukuru Serikali na marafiki wa Sweden ambao wameendelea kutoa msaada katika shule hiyo kwa kuwasomesha wasichana wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
Naye Mwenyekiti na Mwanzilishi wa shule hiyo, Profesa Anna Tibaijuka alisema anaishukuru Wizara ya Elimu kwa kuachana na masuala ya kupanga shule 10 bora katika matokeo ya mitihani ya kitaifa na badala yake kuzipatia daraja shule kwa namna zilizofaulisha wanafunzi.
“Ukisema huyu ni wa kwaza unapima nini, hali hii ilizifaya hule nyingi katika masuala ya kuiba mitihani ili waingie katika 10 bora, tunashukuru serikali kuliona hili na kuliondoa, sisi Barbro Johansson tunawajenga wasichana kufaya vizuri wakati wote na kujiamini ndio maana haturuhusu wanafunzi kuchapwa kiboko,” alisema
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo, Jospina Leonidace alisema jumla ya wanafunzi 83 wanahitimu elimu ya kidato cha sita na kwamba wote wanandoto kubwa ya kujiendeleza zaidi kielimu ili waweze kulitumikia taifa.
Alisema wanafunzi hao wamelelewa ili waje kuwa viongozi bora wenye kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa bidii kwani hiyo ndiyo silaha pekee kwao itakayowawezesha kufikia kilele cha mafanikio.