27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kambi ya Tshisekedi yadai kushinda uchaguzi DRC

KINSHASA, DRC

TIMU ya Kampeni ya mgombea urais nchini hapa, Felix Tshisekedi, imesema wawakilishi wa kambi yao wamekutana na kambi ya Rais anayemaliza muda wake, Joseph Kabila kufanya makabidhiano ya amani ya madaraka.

Kambi ya Kabila hata hivyo imekanusha kuwapo na mikutano hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Desemba 30, mwaka jana ambao matokeo yake ya awali yanatarajiwa kutangazwa baadae wiki hii.

Uchaguzi huo ulilenga kuleta mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia nchini hapa katika kipindi cha miaka 59 ya uhuru, lakini wasiwasi unazidi kuenea huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakiituhumu Serikali kwa kujaribu kuiba kura.

Tshisekedi aliwania urais dhidi ya mgombea aliyeteuliwa na Kabila mwenyewe, Emmanuel Ramazani Shadary, na kiongozi mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, ambaye kura za maoni kabla ya uchaguzi huo zilionesha akiongoza kinyang’anyiro hicho.

Ripoti za mawasiliano kati ya kambi za Tshisekedi na Kabila zimezusha shaka miongoni mwa wafuasi wa Fayulu.

Wanahofia kuwa huenda Kabila anajaribu kujadili ugawanaji wa madaraka na Tshisekedi baada ya kuona kile ambacho wanadiplomasia wengi wanaamini mgombea wake Shadary anaburuza mkia katika matokeo.

Kwenye mkutano na wanahabari, Katibu Mkuu wa chama cha Tshisekedi cha UDPS, Jean-Marc Kabund, alisema mawasiliano kati ya kambi mbili yanalenga maridhiano ya kitaifa, na kwamba UDPS inapinga sera yoyote ya kulipiza visasi.

“Viongozi hawa wawili (Kabila na Tshisekedi) wana masilahi katika kukutana kuandaa mazingira ya amani na ya ustaarabu ya kukabidhiana madaraka,” alidai Kabund.

Hata hivyo, Msemaji wa Tshisekedi, Vidiye Tshimanga, alisema Kabila na Tshisekedi hawajakutana ana kwa ana, lakini kwamba wawakilishi wao wamekutana mara kadhaa.

Kabila anatazamiwa kuachia ngazi baadae mwezi huu baada ya kukaa madarakani kwa miaka 18.

Kukataa kwake kuondoka wakati muhula wake ulipomalizika rasmi mwaka 2016 kulisababisha maandamano ambayo vikosi vya usalama viliua watu wengi.

Hata hivyo, Barnabe Kikaya bin Karubi, mmoja wa washauri wa Kabila na msemaji wa Shadary, alikanusha kuwapo mawasiliano yoyote na Tshisekedi au wawakilishi wake.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku ya Jumanne, muungano wa vyama tawala umeituhumu kampeni ya Fayulu na maaskofu kwa kujaribu kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi katika taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini.

Wiki iliyopita, maaskofu hao walisema wanajua mshindi wa uchaguzi, tangazo lililotazamwa na wengi kama onyo kwa mamlaka dhidi ya wizi wa kura.

Kabund alimtaja Tshisekedi kama mshindi wa uchaguzi huo, lakini hakusema alikuwa anajengea hoja yake kwa msingi gani.

Kambi ya Shadary ilisema inatarajia kushinda huku ile ya Fayulu pia ikisema alikuwa katika nafasi imara ya kuibuka kidedea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles