25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

Kamati za Bunge kizaazaa

Kamati za Bunge kizaazaa*Zitto, Heche, Sakaya wazirarua, Mtatiro ahoji watakaochaguliwa PAC kama wataweza kuvaa viatu vya ZZK

*Wabunge CCM wapongeza, mwingine awaponda wapinzani awaita malofa

* Chenge, Aerukamba, Ghasia wapewa uennyekiti wa kamati

NA WANDISHI WETU

KITENDO cha wabunge machachari wa upinzani ambao wanasifika kwa uwezo wa kujenga hoja na kusimamia ukweli wa mambo kutoswa katika Kamati nyeti za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na badala yake wakajumuishwa kwenye kamati moja ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kimezidi kuibua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge.

Kuibuka kwa hali hiyo kunatokana na kile ambacho wengi wamejenga hisia kwamba uongozi wa Bunge umefanya uteuzi huo kwa kushirikiana kwa siri na Serikali ili kupunguza nguvu ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Wapo ambao wamekwenda mbali na kuutupia lawama uongozi wa Bunge kuwa huenda umechukua uamuzi huo kwa shinikizo la chama tawala cha CCM ambacho kipo katika mkakati maalumu wa kurejesha nguvu yake ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 baada ya kuonja machungu ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Imeelezwa kuwa pamoja na kupata ushindi wa urais na kuongoza kwa viti vya ubunge, CCM kiliathirika kisiasa kutokana na nguvu ya muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi  mkuu wa mwaka jana.

Kwamba chama hicho kimetumia nguvu yake kupitia mgongo wa Serikali kuweka msukumo kwa uongozi wa Bunge kuhakikisha wabunge machachari wa upinzani hawapati nafasi ya kusimamia kamati za PAC na LAAC ambazo kwa namna moja au nyingine zinatajwa kuwa ni majukwaa ambayo wapinzani waliyatumia kujiimarisha.

Kwa muktadha huo, wafuatiliaji wa mambo wanakitazama kitendo hicho cha Bunge kuwa ni sawa na kushindwa kujisimamia lenyewe na badala yake limetoa mwanya kwa Serikali kupenyeza mambo yake ndani ya mhimili huo.

Kutokana na hali hiyo, mwanasiasa na mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, akihojiwa jana jioni na kituo cha Televisheni cha East Africa alisema haitoshi tu kusema kwamba wapinzani wamepangwa katika kamati ya PAC lakini je, watakaochaguliwa kuongoza kamati hizo wataweza kuvaa viatu vya Zitto Kabwe?

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) katika ukurasa wake wa Facebook aliandika ujumbe akidai upangaji wa kamati za Bunge umelenga kukifanya chombo hicho kusimamiwa na Serikali badala ya Bunge kuisimamia Serikali.

“Kamati ya PAC ambayo kanuni inasema itaongozwa na upinzani, wamewekwa Ukawa sita na CCM saba, Kamati ya Ukimwi Ukawa 11 na CCM 12, ukiangalia kamati ya LAAC ambayo ni Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, CCM wako 16 na Ukawa sita ..itakumbukwa pia kwa mujibu wa kanuni kamati hii inaongozwa na upinzani,” alisema Heche.

Aliongeza kuwa kwenye kamati ya bajeti na kwingine, wabunge wengi wenye uzoefu na uwezo na ambao wangeisaidia nchi wameondolewa.

Mbali na hoja hiyo ya Heche, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, aliandika katika mitandao ya kijamii pamoja na mambo mengine akieleza fitina kama msingi wa wabunge tishio wa upinzani kukosa kupangwa katika kamati nyeti.

Katika andiko lake hilo ingawa Zitto anasema kamati zote za Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge na kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati yoyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine, lakini akahoji kile alichodai kupindishwa kwa kanuni ambazo zinaweka utaratibu wa uteuzi kwenye kamati ikiwemo maombi ya wabunge, uzoefu na ujuzi wa eneo husika.

“Hivyo wanaolalamikia upangaji wa kamati ndio usiku wa kuamkia jana (juzi) walimshinikiza Spika asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye kamati wanazoona wao ni nyeti.

“Ni unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la mbunge na ujuzi wakati huo huo wenye vigezo vyote hivyo unawapiga vita kwa sababu za kisiasa…Ni dhahiri kuwa mpangilio wa kamati unajenga Bunge kibogoyo. Nilitahadharisha toka Bunge la 11 lilipoanza kwamba kuna dalili za Serikali kutaka kulidhibiti Bunge (kumbukeni sarakasi za Tulia Ackson ambaye sasa ni Naibu Spika),” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa unapokwenda kwa Spika kusema ‘fulani asipangwe kamati fulani kwa sababu atapata sifa halafu ukataka ‘nyumbu’ wako ndio wapangwe huko ujue unaisaidia Serikali kudondosha Bunge.

Alisema Spika anapoamua huyo usiyemtaka na nyumbu wako wasiende huko ujue amekudharau.

“Unapoona viongozi wa Serikali wanahangaika kupanga kamati za Bunge watakavyo wao ujue viongozi hao dhaifu  hawana nia njema na kuwajibishwa …twendeni kwenye hizi kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania. Twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki Bunge tu na wabunge tusikubali Bunge kibogoyo.”

“Ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na Malaika. Serikali ni chombo cha mabavu lazima idhibitiwe na ndiyo kazi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alisema ameridhishwa na uundwaji wa kamati hizo.
Maige ambaye amepangwa kwenye kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema wanaopinga kamati hizo ni malofa.
“Mimi nimewekwa kwenye kamati kama nilivyoomba. Tatizo wengi tulidhani tutapelekwa kwenye kamati bila kujali idadi. Kwa mfano wewe ni mhandisi na mmeomba kamati ya miundombinu wahandisi wote, je, mtapangwa wote? Spika ametumia busara kupanga kama alivyofanya,” alisema Maige na kuongeza:
“Ili mtu kupendekezwa ni utaratibu tu, lakini mbunge anaweza kuwekwa popote. Kwani kuna kamati ambayo haiwasaidii wananchi?… Sisi kwenye kamati ya PAC tumeleta heshima kwa kambi ya upinzani kwa kuacha nafasi ya mwenyekiti, asipokuja tunaendelea tu kuchapa kazi, wanaopinga ni malofa…”
Naye Mbunge wa Rufiji, Abdallah Ulega, alisema ameridhishwa na uundwaji wa kamati hizo.

Maelezo hayo ya Ulega hayakupishana na kauli aliyotoa Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis ambaye aliunga mkono uundwaji wa kamati hizo licha ya kutopata kamati aliyoomba.
“Mimi nimeridhishwa na uundwaji wa kamati hizo licha ya kwamba sijapata kamati niliyoomba. Ni lazima tuheshimu uamuzi wa kiti cha Spika,” alisema Sadifa.
Mbunge wa Kilombero, Susan Kiwanga, alisema kilichofanyika katika upangaji wa kamati ni ukandamizaji.
“Kilichofanyika ni kutukandamiza, kwa sababu upangaji uliopo hauna manufaa yoyote kwa wapinzani,” alisema.
Naye Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya, alisema kulikuwa na mkakati wa kuwabana wapinzani na hawatakubaliana na mkakati huo.
“Siku zote wamekuwa wakifanya njama za kukandamiza upinzani kwa kuchomeka wabunge wa upinzani wanaowataka katika kamati za PAC na LAAC. Tatizo haturuhusiwi kupendekeza majina ya wajumbe wa hizi kamati kwa hiyo wanaweka watu wanaowataka wao ili wawaburuze,” alisema Sakaya na kuongeza:
“Safari hii hatutakubali pamoja na uchache wetu lakini kuna mambo mengi tumeshayafanya na tumefanikiwa. Hata kwa hili tutafanikiwa na ulimwengu wote utajua.”
Katika hatua nyingine Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, aliandika ujumbe mfupi katika mtandao wa Twitter akisema kuwa upinzani uchwara hushamiri sana wakati wa Serikali dhaifu lakini upinzani makini huibuka wakati Serikali makini na yenye chembe za udikteta.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu wa Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Bunge lina kanuni zake za uteuzi wa kamati na anaamini kanuni hizo zimetekelezwa kupata wajumbe wa kamati zote za Bunge la 11.

Alisema haoni mantiki ya wabunge kuonyesha wasiwasi wa uteuzi huo kwa sababu nguvu yao ya kibunge inasimama kwa hoja watakazozitoa bungeni kwamba hoja binafsi ya mbunge inaweza kusimama na kuongoza ajenda ya kamati husika.

“Sidhani kama kamati ni jukwaa la kutafutia umaarufu kama wengi wanavyofikiri, pia kamati haiwezi kuwa juu ya kanuni za Bunge ndiyo maana wanateuliwa na Bunge, hawa wanaolalamika kuwa kamati nyeti hazina wazoefu wanataka kuwa wafalme wa kamati za Bunge?

“Kama usimamizi wa Serikali mbunge anaweza kusimama kwa hoja yake binafsi kama alivyofanya Kafulila ambapo matokeo yake yalionekana baada ya PAC kuchunguza na kubaini yale Kafulila aliyoyalalamikia,” alisema Dk. Bana.

Pia alisifu uteuzi wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kujaza vijana wanaochemka kiakili na wenye uwezo wa kuhoji mambo.

“Hii kamati watu wanaipuuza lakini hawaijui tu, hii ndiyo kamati nyeti ambayo inasimamia mambo mengi ya Serikali yanayotumia mabilioni ya fedha, naamini kabisa vijana walioteuliwa katika kamati hii wataibua mengi kuliko inavyodhaniwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,682FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles