24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati yapendekeza vyanzo vingine vya mapato bajeti kuu

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KAMATI ya Kudumu ya Bajeti imetaja maeneo muhimu ambayo yatasaidia kupatikana kwa vyanzo vipya vya mapato, ikiwemo urasimishaji wa sekta isiyokuwa rasmi.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Simbachawene, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20 pamoja na tathmini ya utekelezaji  wa bajeti ya Serikali  kwa mwaka 2019/20.

Simbachawene alisema kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na shughuli ambazo hazipo katika mfumo rasmi, hivyo kusababisha ugumu katika kuzilea ili zikue na baadae kuchangia katika mapato ya kodi.

“Kamati inaamini kwamba hatua hizo zikikamilika zitarahisisha utambuzi kwa nia njema ya kujenga na kuendeleza sekta isiyo rasmi ili iweze kukua na mchango kuonekana katika pato la taifa,” alisema.

Pia alitaja eneo jingine kuwa ni katika huduma za kifedha ambapo kamati imeishauri Serikali kuziongezea mtaji Benki ya Kilimo (TIB) na Benki ya Rasilimali (TADB).

“Uwekezaji katika sekta ya viwanda na sekta ya kilimo, hasa kilimo cha mazao ya biashara, huhitaji fedha nyingi na kuchukua muda mrefu kutoa faida na umegubikwa na vihatarishi vingi.

“Ukweli huu umepelekea maeneo haya kutokuwa na mvuto kwa benki zingine za biashara katika utoaji wa mikopo ambayo ingesaidia sana katika uwekezaji.

“Ni maoni ya kamati kuwa Benki ya Rasilimali na ya Kilimo zinapaswa kuwa njia thabiti ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya sekta hiyo muhimu. Kamati inashauri Serikali kuziongezea mtaji benki hizo ili ziweze kutoa mikopo,” alisema.

Alitaja chanzo kingine ni kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi ili iweze kushiriki katika utekelezaji wa miradi iliyoainishwa katika mpango wa maendeleo.

Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe (CCM), alitaja chanzo kingine ni kwenye diplomasia ya uchumi.

“Eneo hili ni muhimu katika kusaidia Serikali kupata mapato kupitia uhamasishaji wa vivutio vilivyopo ili kupata wawekezaji wa kigeni kwenye sekta ya kilimo, uvuvi, utalii, miundombinu, biashara  na huduma,” alisema.

Katika hatua nyinge, Kamati imeishauri Serikali ihakikishe inaunganisha taasisi zote zenye majukumu yanayofanana (OSHA, TBS, TFDA, Fire) ili kurahisisha  utekelezaji katika maeneo mbalimbali.

“Serikali iweke mkakati wa kuvilinda viwanda vya ndani ambayo yatavutia viwanda hivyo kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kuzalisha nchini kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje,” alisema.

Kama hiyo pia ilishauri Serikali kuhuisha mifumo ya utambuzi kwa kutumia aina moja ya kitambulisho  badala ya kuweka kwa mifumo mingi inayofanya kazi zinazofanana.

UPINZANI 

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alisema bajeti mbadala ya kambi hiyo itakuwa ni ya zaidi ya Sh trilioni 29.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba (Chadema), alisema vipaumbele katika bajeti yao ni sekta za elimu ambayo imetengewa  zaidi ya Sh  trilioni 4, kilimo zaidi ya Sh trilioni 5, viwanda zaidi ya Sh trilioni 4, maji zaidi ya Sh trilioni 2, afya zaidi ya Sh trilioni 2 na mengineyo Sh trilioni 8.

Pia kambi hiyo ilidai kwamba bajeti ya Serikali imejikita kwenye maendeleo ya vitu na sio ya watu.

Silinde pia alidai kwamba mfumo wa ulipaji kodi umekuwa ukilalamikiwa kwa miaka mingi na wafanyabiashara ambao ndio huwa wanalipa kodi, hivyo mfumo huo sio shirikishi.

“Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa pendekezo,  kutokana na kuendelea kupungua  kwa makusanyo ya kodi licha ya Serikali hii ya awamu ya tano kutumia mbinu nyingi za kukusanya mapato, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kikosi maalumu cha kukusanya kodi,” alisema.

Pia kambi hiyo ilisema kwamba usimamizi  ni dhaifu katika usimamizi wa deni la taifa.

“Kwa mfano ukaguzi wa CAG ulibaini mapungufu yatokanayo  katika usimamizi wa deni la taifa,” alisema Silinde.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), aliiomba Serikali kuwasaidia wakulima wa zao la pamba kutokana na wanunuzi kujipangia bei.

“Tuache siasa katika zao la pamba, tunawanyanyasa wakulima, kwenye zao la pamba misimu yote unapotaka kuanza msimu wa pamba mara unasikia umepanda, unasikia wanauza 1,400 mpaka 1,500. Serikali iingilie kati hii sio bure, wanunuzi wanataka kuwaibia wananchi,” alisema Ndassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles