24.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 25, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kamati ya Bunge yataka kuongezwa huduma za kijamii Soko la Kariakoo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeiagiza Serikali kuongeza maeneo ya huduma za kijamii katika Soko la Kimataifa la Kariakoo ili kurahisisha shughuli za kibiashara kwa watu wanaoingia sokoni hapo.

Maagizo hayo yametolewa Februari 21,2025 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo, baada ya kutembelea soko hilo pamoja na eneo lilipoanguka jengo la ghorofa mwishoni mwa mwaka jana na kuua watu 30.

Kamati hiyo imependekeza kuwe na sehemu ya kutolea huduma za afya, sehemu maalumu ya kunyonyesha watoto, chumba cha kinamama kwa ajili ya kubadilisha taulo za kike na kituo cha malezi ya mchana (day care) kwa kina mama wanaokuja na watoto kazini.

“Tumeridhishwa na hatua za ujenzi wa soko, kazi kubwa imefanyika lakini tunashauri kuwe na huduma ya afya kwa sababu soko linachukua watu wengi ili ikitokea dharura iwe rahisi mtu kusaidiwa. Kuwe pia na kituo cha ‘day care’ hii itasaidia kwa kinamama wanaokuja na watoto kazini,” amesema Kyombo.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Mary Maridadi, amesema mpaka sasa wafanyabiashara 1,159 kati ya 1,520 ambao wanapaswa kurejea tayari wamerejesha fomu na wanaendelea na hatua mbalimbali za uchambuzi.

Aidha amesema wameunda timu kupitia malalamiko ya wafanyabiashara ambao wanadai walikuwepo kabla soko halijaungua na kudokeza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha baadhi yao walikuwa wameuza maeneo na wengine hawakujitokeza wakati wa uhakiki.

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Amani Mafuru, amesema soko jipya litakuwa na mita za mraba 40,000 na nafasi za biashara zaidi ya 3,000 kutoka 1,600 za awali ambazo zitatosha wafanyabiashara wote waliokuwepo na wengine watakaoomba.

Soko la Kariakoo liliteketea kwa moto Julai 10,2021 na kuteketeza mali za wafanyabiashara zilizokuwemo na Serikali imetoa Sh bilioni 28 kulikarabati ambapo ujenzi umefikia asilimia 93.6 na linatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles