ASHA BANI Na MAMII MSHANA (TUDARC)
-DAR ES SALAAM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imekubaliana na uamuzi wa Serikali wa kutumia mashine zilizounganishwa kwenye mfumo wa kielektroniki, ambazo zina uhakika katika ukusanyaji wa mapato katika kivuko cha Feri, Dar es Salaam.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, alipokuwa akizungumza na watendaji wa Kampuni ya Maxcom Africa Plc, baada ya kukagua mfumo huo wa malipo.
Alisema mfumo huo wa ukusanyaji mapato unakwenda sambamba na matarajio ya Bunge ya kutaka kuwe na udhibiti katika makusanyo ya fedha za Serikali kuliko ilivyokuwa awali.
Ghasia alisema kabla ya kuanza kwa mfumo huo, taarifa zilionyesha kuwa idadi ya watu waliokuwa wakitumia kivuko hicho ilikuwa ndogo ingawa baada ya kipindi cha majaribio tangu ulipofungwa mfumo wa kieletroniki imebainika watu 200,000 hutumia kivuko hicho kwa siku.
“Kamati imekubali mpango wa Serikali wa kutumia mashine za kielektroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa nauli kwenye kivuko cha Feri, lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunapunguza mianya ya upotevu wa fedha na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yalikuwa yakihujumiwa na wajanja,” alisema Ghasia.
Awali akitoa maelezo kuhusu mfumo huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Maxcom Africa Plc, Jameson Kasati, alisema kuwa unapunguza upotevu wa mapato ya Serikali kwa sababu kila fedha inayokusanywa inaonekana kwenye mfumo rasmi.