30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya Bunge ya Bajeti yaridhishwa na miradi ya maendeleo pori la akiba Mkungunero

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Daniel Sillo imefanya ukaguzi wa miradi mitatu ya uboreshaji wa miundombinu ya kitalii iliyopo katika Pori la Akiba la Mkungunero lililopo katika mikoa ya Dodoma na Manyara.

Ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa miradi ya ujenzi ya barabara yenye kilometa 47.5, lango kuu la kuingilia wageni na eneo la kupumziki watalii “picnic site” yote ikigharimu kiasi cha Sh milioni 672.

Miradi hiyo imejengwa kwa kupitia fedha za Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

Ukaguzi huo umefanyika Julai 5, 2022 ambapo akizungumza mara baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti, Daniel Sillo amemshukuru, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo.

Aidha, Sillo ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na akasisitiza kuendelea kusimamia matumizi mazuri ya fedha za miradi ya maendeleo.

“Niwapongeze Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAWA kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kuimarisha miundombinu ya barabara, pia eneo la kupumzikia wageni na sehemu nyingine kwani hii itasaidia kuchochea ongezeko la watalii.

“Pia kwa mara nyingine nimpongeze Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwani kupitia jitihada zake za kutuletea fedha za Uviko-19 ambazo zimeendelea kuchochea maendeleo nchini kwetu. Wito wangu kwenu, simamieni vizuri fedha za umma, ili zilete tija kwa kizazi cha sasa na baadae,” amesema Sillo.

Awali, akizungumza wakati wa ukaribisho, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema uboreshaji wa miundombinu katika Pori la Akiba Mkungunero utatoa wigo mpana wa eneo hili kutembelewa na watalii kwa sababu ya miundombinu inayoendelea kuwekwa.

Pia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameipongeza TAWA kwa nzuri na aliishukuru kamati kwa kutenga muda kwa ajili ya kupitia miradi hiyo.

Naye, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange amemshukuru, Rais Samia kwa kutoa fedha hizi ambazo zimetolewa kwa kipindi muafaka wakati Taifa likijiandaa kupokea wageni wengi baada ya uzinduzi wa filamu maalumu ya “Royal Tour”.

Aidha, Kabange ameishukuru kamati na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles