23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

Kamati kuchunguza kashfa wanafunzi kupewa mimba

 GAUDENCE MSUYA– NANYUMBU

MKUU wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Moses Machali ameahidi kuunda kamati kuchunguza kashfa ya wanafunzi wa shule ya msingi kupewa mimba na madai kwamba walimu wamekuwa wakiwatuma kuwanunulia kondomu.

Uamuzi huo umekuja baada ya wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nandete kumwandikia barua Machali wakitaka ufanyike uchunguzi kuhusu kashfa ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kushirikiana na mratibu wa elimu kata kufumbia macho matukio ya mimba na kisha kuchukuliwa hatua stahiki.

Machali alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, aliyetaka kujua kama malalamiko hayo yamefikishwa ofisini kwake na hatua gani atachukua ili wananchi wa eneo hilo waweze kuishi kwa amani.

Alisema ameshapokea malalamiko yahusuyo sekta ya elimu kutoka kwa wazazi wa wanafunzi wa Kata ya Nandete waliolalamikia mambo mawili ambayo ni kashfa ya baadhi ya walimu kudaiwa kuwatuma wanafunzi wakawanunulie kondomu na nyingine ya uongozi wa shule na mratibu elimu kufumbia macho malalamiko ya mimba za wanafunzi. 

“Malalamiko hayo nimeyapokea na nitahakikisha naunda kamati ya kwenda kuchunguza, watakaobainika kuhusika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kuadhibiwa kiutumishi,” alisema Machali.

Awali wakazi wa Kijiji cha Nandete walilalamika kwamba wanafunzi wanaporejea majumbani kwao wamekuwa wakiwalalamikia kwamba baadhi ya walimu huwatuma wakawanunulie kondomu madukani. 

“Hivi inakuwaje mwalimu anamtuma mwanafunzi akamnunulie kondomu dukani, kwanini asiende kununua mwenyewe, na hili linajirudia mara kwa mara na hata tukienda kwa mwalimu mkuu kulalamika anasema tunampelekea majungu,” alilalamika Husna Ali.

Mbwana Baraka alisema pia kuna wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Nandete wamepewa mimba, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliowapa mimba licha ya kufikisha malalamiko kwa mwalimu mkuu na mratibu elimu.

“Baada ya kuona hatusikilizwi ngazi ya kata, tumeamua kumwandikia barua Mkuu wa Wilaya tukiamini kwamba malalamiko yetu yatafanyiwa kazi na wanafunzi wetu watapata elimu bila kusumbuliwa,” alisema Baraka.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Nandete, Hashimu Yahaya na Mratibu Elimu Kata ya Nadete, Hashim Naweka walipoulizwa na mwandishi wa habari hii kuhusu malalamiko haya, walisema hawaruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari na kwamba msemaji ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nanyumbu.

“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na malalamiko hayo, hata mimi nayasikia kwako, lakini ukweli ni kwamba utaratibu unaeleweka, mimi siyo msemaji bali ni hadi kibali cha mkurugenzi wa halmashauri yetu ambaye ndiye bosi wangu,” alisema Naweka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles