30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Kamanda Shilogile atoa ushahidi kesi ya Ponda

ponda1Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustin Shilogile, amepanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kutoa ushahidi dhidi ya Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa.
Shilogile alipanda kizimbani jana ambako katika kutoa ushahidi wake aliongozwa na wakili wa serikali, Juma Nosor.
Akimuongoza Shilogile katika kutoa ushahidi wake, Nasoro alianza kwa kumuhoji: Umekuja mahakamani kufanya nini leo ?.
Shahidi (Shilogile): Nimekuja kutoa ushahidi kuhusu kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda .
Wakili: Kesi ya nini ?
Shahidi: Inayomkabili mahakamani hapa.
Wakili: Shahidi wewe ni ofisa mkubwa wa Jeshi la Polisi, mbona unajibu maswali kienyeji?
Shahidi: Najibu ninavyojua mimi usinilazimishe kujibu unavyotaka wewe na ni kweli mimi ni ofisa wa jeshi la polisi mkubwa, siyo uongo.
Wakili: Je? unafahamu juu ya uchochezi wa Sheikh Ponda?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili:Je, unafahamu kuwa hukumu ya Kisutu dhidi ya Sheikh Ponda imetenguliwa?
Shaidi: Sifahamu.
Wakili: Kamanda Shilogile unafahamu kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi?
Shahidi:Sifahamu kama alipigwa risasi ninachojua mimi kuwa alipigwa na kitu chenye ncha kali.
Wakili: Je, baada ya Sheikh Ponda kujeruhiwa jeshi la polisi mlichukua hatua gani?
Shahidi: Tulikwenda hadi hospitali ya mkoa na tulipofika tuliambiwa kuwa Sheikh Ponda alifika hapo na kuondoka.
Wakili: Je, shahidi unakumbuka mara baada ya tukio la Sheikh Ponda ulizungumza na vyombo vya habari vikiwamo vya ndani na nje ya nchi kama BBC na unakumbuka uliyozungumza kwenye vyombo vya habari?
Shaidi: Sikumbuki.
Wakili: Kwani jeshi la polisi mna utaratibu wa kuandika tarehe za nyuma za matukio?
Shahidi: Hayo ni mawazo yako.
Wakili: Je, OCD alikuja ofisni kwako akiwa tayari ameshatoa kibali cha kongamano la akina Sheikh Ponda?
Shaidi:Nilipokea nakala ya kuomba kufanya kongamano tarehe Mosi mwaka huo siyo taarifa ya kibali.
Wakili: Je, mara baada ya kupokea taarifa ya kongamano walikwambia kuwa Sheikh Ponda ni mgeni mwalikwa katika kongamano?
Shahidi: Ndiyo lakini yeye alikuwa mgeni mwalikwa na siyo msemaji mkuu katika kongamano hilo.
Wakili: Je, una taarifa yoyote kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi au bomu la machozi?
Shahidi: Sina taarifa.
Wakili: Je, OCD alikutaarifu nini juu ya Sheikh Ponda siku hiyo?
Shahidi: Alinitaarifu kuwa Sheikh Ponda alipanda jukwaani saa 11:45 jioni.
Wakili: Je, amri yako ya kutaka Sheikh Ponda akamatwe ilitoka kwa ajili ya kuambiwa kuwa Sheikh Ponda alikuwa mwalikwa na siyo msemaji katika kongamano hilo?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Kwa hiyo unadhani amri ilitoka Zanzibar au makao makuu?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili: Je, unamfahamu Aduvela Senso?
Shahidi: Ndiyo ni msemaji wa jeshi la polisi Tanzania.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Bernald Kongola alimuomba hakimu ili waweze kutoa ushahidi wa video ya matukio yote na ushahidi huo ulitolewa na mtalaamu wa kitengo cha teknolojia ya habari (IT) cha jeshi la polisi.
Baada ya video hiyo kuonyeshwa mahakamani baadhi ya wafuasi wa Ponda walionekana kububujikwa na machozi.
Hadi tunakwenda mitamboni kesi hiyo ilikuwa inaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles