KAMA UTANI VILE… TUNAMSAHAU GODZILLA

0
715

Na RAMADHANI MASENGA

MSANII Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego anaamini msanii Billnass ni mbadala wa Godzilla. Ila wadau wanapinga. Wanasema mbali na ukali wa Billnass ila ni kumkosea heshima King Zilla kumfananisha naye. Huo ndiyo ukweli unaoaminiwa na wengi.

Ila kabla hujahoji ni kwanini Ney anasema pengo la Godzilla ni Billnas, jiulize huu ujasiri Ney kaupata wapi? Ney kweli akisikiliza kwa makini nyimbo za Godzilla anaona zinaweza kufanana na za Billnass? Usiamini kuwa Ney ana matatizo ya masikio.

Huu ujasiri wa Ney unakuja baada ya Godzilla kuonekana kama ameamua kuwa Godzilla tu asiye na yale madhara aliyowahi kuwa nayo zamani. Siku hizi unamsikia sana Godzilla? Hapana. Sababu? Hakuna anayejua.

Huenda kuna genge linataka kumkwamisha, ila je anafanya nini kuonesha makali yake hata kwa njia ndogo anayopata?

Godzilla anaonekana kama yupo katika dimbwi la msongo wa mawazo. Msikilize katika mahojiano yake. Muone hali atakayokutana nayo pindi ukimuona. Katika mahojiano yake haonekani kuwa serious sana.

Anahojiwa Kiswahili anajibu kwa Kiingereza. Hajali kitu. Kila muda ni kama kalewa vile. Sio bure. Godzilla huyu sio yule ambaye tulikuwa tunamjua.

Godzilla wa kipindi kile japo alionekana kupenda pombe ila alionekana kuwa na staha na nidhamu katika mahojiano aliyofanyiwa na wanahabari. Alikuwa anajua mahojiano yanaweza kumpa heshima ama kuibomoa heshima yake.

Akawa anachagua kujenga heshima yake kwa maneno makini yenye kueleweka. Alitulia katika mahojiano, alijibu kimkakati na kuwa na heshima na wana habari. Ila Godzilla wa sasa hayuko hivyo.

Anajibu kama vile mtangazaji anamsumbua. Anaongea kana kwamba mahojiano yake yataishia Salasala, katika ghetto za masela wake.

Kuna haja ya kufanya jitihada za makusudi ili kumsunuru Godzilla – ana kipaji kikubwa sana. hafikiwi na Billnas wala John Makini. Kama mdau mmoja makini atakaa naye na kumwambia thamani ya kipaji chake kwa kina, nina imani King Zila atabadilika.

Zilla hana shida kubwa. Ni msongo wa mawazo wa kuona watu, tena waliokuwa marafiki zake wamemgeuka na kuacha kucheza nyimbo zake. Akili ya Godzilla imekataa kukubaliana na hali hii ili kuifanya kuwa changamoto ya kufanikiwa.

Ni kama kaona mwisho wa muziki wake. Kwa ukubwa wa kipaji cha chake hatakiwi kuwa hivi. Mpaka sasa Godzilla ni miongoni wa wakali halisi wa freestyale. Aheshimu uwezo wake huu kwa sababu hauko kwa wasanii wengi wajiitao wakali wa Hip Hop.

Niki Mbishi ni miongoni mwa wakali ambao wanatajwa kubaniwa nyimbo zao. Ila umewahi kumuona anavyokuwa akihojiwa na waaandishi wa habari?

Anakuwa mtulivu, mwenye busara na kuweka malengo yake hadharani. Anajua japo nyimbo zake hazipigwi sana katika baadhi ya vituo vya  redio na televisheni kwa sababu tofauti, zikiwemo na zile za kijinga ila anaweza kuingiza chochote kupitia kuuza nyimbo mitandaoni.

Zilla anatakiwa kumuiga kaka yake huyu. Kwa miaka mingi Niki anaitwa mkali ila nyimbo zake hazitambi redioni. Mameneja na wa watangazaji fulani kwa sababu zao hawataki kumsapoti.

Ila hakati tamaa. Bado anaandika mistari mikali,  anaonekana majukwaani na bado mtaani ana heshima kubwa.

Kisa kubaniwa na watu fulani kudhani muziki umeisha, hayo siyo matumizi sahihi ya akili. Zilla ni miongoni mwa watu wenye kutajwa kuwa na upeo mkubwa wa mambo.

Katika kipindi hiki kigumu kwake ndipo upeo wake unapotakiwa kutumika kumvusha salama. Kunywa tu pombe pamoja na kujiweka katika mazingira ya kukata tamaa, siyo tu anawaangusha mashabiki wake ila pia anajipeleka katika shimo la kushindwa kwake kimaisha na kimuziki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here