27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KAMA GADDAFI ALIANGUKA, KINA JAMMEH NAO WATAANGUKA

mugabe

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

MWAKA mpya umewadia baada ya mawio na machweo ya mwaka jana. Kuanza kwa mwaka mpya ni kuanza upya kwa safu hii ya kisa mkasa. Kwa kuanzia, narejea ziara ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, aliyoifanya mwaka 2014 nchini China.

Katika ziara hiyo ya kikazi, Kikwete alizungumza na mabalozi wa Afrika waliokuwa wakiziwakilisha nchi zao China.

Pamoja na mambo mengine, alisema anasubiri muda wake wa kukaa madarakani ufikie kikomo ili akapumzike na kulea wajukuu zake katika Kijiji cha Msoga kilichopo Chalinze mkoani Pwani.

Alisema wakati mwingine kuna baadhi ya watu wanawashawishi viongozi wang’ang’anie madaraka kwa kuwa wananufaika nao. Baada ya kutoa kauli hiyo, mabalozi hao walimshangaa Kikwete kwa kuwa wanafahamu namna baadhi ya marais wa Afrika wanavyong’ang’ania madaraka.

Kweli Kikwete kapumzika na utawala wa nchi kamwachia Rais Dk. John Magufuli, lakini bado kuna baadhi ya marais wa Afrika wameng’ang’ania madaraka na wengine hawataki kuyaachia.

Miongoni mwao yupo Rais wa Gambia, Yanya Jammeh, anayeng’ang’ania madaraka licha ya kukubali kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Desemba, mwaka jana na mpinzani wake, Adama Barrow, kuibuka mshindi.

Kitendo cha Jammeh kukataa kukabidhi madaraka kwa Barrow, kimepingwa nchini mwake na katika majukwaa ya kimataifa lakini hiyo haijasaidia kitu na amekuwa akiendelea kusimamia msimamo wake kuwa kura zilihesabiwa vibaya na akatoa amri uchaguzi urudiwe.

Hali hiyo imeleta taharuki kwa baadhi ya wananchi wa Gambia walioona kama mwisho wa utawala wa mabavu wa zaidi ya miongo miwili ulikuwa umekamilika.

Rais mwingine aliyeng’ang’ania madaraka ni Pierre Nkurunziza wa Burundi baada ya kugombea kwa mara ya tatu mfululizo na kushinda Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Juni, mwaka juzi.

Licha ya kupingwa na jumuiya za kimataifa, wanaharakati na wapinzani wake wa ndani lakini akagombea urais kwa hoja kwamba utawala wa awamu yake ya kwanza ulikuwa wa mpito! Eti alisema kwamba katika muhula wake wa kwanza aliitawala Burundi kupitia Katiba ya zamani kwa hiyo kupitia Katiba mpya bado ana muhula wake wa pili ambao ni wa mwisho.

Baada ya uchaguzi huo, visa vya baadhi ya Warundi kuendelea kuuawa viliendelea kushamiri na kusababisha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Fatou Bensouda, kuibuka Aprili, mwaka jana na kusema atachunguza ghasia za Burundi.

King’ang’anizi mwingine ni Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyetaka kugombea tena kwa mara ya tatu mfululizo licha ya kutokuwa na sifa kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo hatua ambayo imesababisha Tume ya Uchaguzi nchini humo kutangaza kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu hadi Julai, mwaka huu na kumwacha aendelee kuongoza.

Uamuzi wa uchaguzi huo kuahirishwa ulitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya DRC, Corneille Nangaa.

Hatua ya Kabila kung’ang’ania madaraka imesababisha mvutano baina yake na wapinzani na kuleta machafuko, maandamano na kusababisha vifo vya mamia ya raia wa nchi hiyo.

Si hao tu, pia Rais Robert Mugabe, naye hana nia ya kuachia madaraka licha ya umri kumtupa mkono baada ya mwaka jana Chama cha ZANU-PF kutangaza kumpitisha kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Huku uchumi wa nchi hiyo ukiwa umedorora na Wazimbabwe wengi wanaogelea katika tope la umasikini.

Kuna sababu kadhaa zinazowasukuma marais hao kufanya hivyo na kubwa kuliko zote ni kuingia madarakani kwa kutumia bunduki na wengine kwa udanganyifu wa matokeo kila uchaguzi unapofanyika.

Ukiitazama historia ya Kabila na Nkurunziza, kuna mahala utaona walishika nafasi hizo baada ya mapambano ya msituni kwa kutumia bunduki na mabomu dhidi ya tawala zilizokuwa madarakani.

Kwa hiyo kuingia kwao madarakani kwa kutumia maguruneti na kumwaga damu kumewafanya kujigeuza ni miungu watu na wana imani kwamba bila wao mambo hayatakuwa sawa katika nchi zao na wamesababisha kuwe na matabaka mawili ya wanaofaidika na wasiofaidika na uongozi wao.

Pia, wanaogopa pindi watakapoachia madaraka mapema vibao vitawarudia kwa kuwa madhila waliyowafanyia wananchi wao ni makubwa.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana katika nchi hizo jirani na Tanzania watu wote wanaonekana ni tishio kwa marais hao ‘wanashughulikiwa’ ipasavyo kuhakikisha harakati zao zinadhibitiwa.

Kimsingi, utawala wao unanikumbusha ule wa Kiongozi wa Libya, marehemu Kanali Muammar Gaddafi, aliyekuwa jasiri, tajiri, jeuri na mbabe kuliko marais hao wanne.

Aliiongoza Libya kwa ‘mkono wa chuma’ na hakutaka akosolewe lakini alikuwa na sifa nyingine upande wa pili tofauti na marais hao wanne ambayo ni kuwajali Walibya katika huduma zote muhimu.

Chini ya Gaddafi, Libya haikuwa na shida ya fedha, umeme, maji, mafuta, afya, elimu wala chakula.

Inadaiwa kuwa wakati wa uongozi wake vijana waliotaka kufunga ndoa walitoa taarifa katika ofisi za Serikali za Mitaa yao kisha waligharamiwa shughuli zote za harusi zao na walipewa fedha za kuanzia maisha.

Walibya hawakulalamikia ugumu wa maisha. Pengine ndiko mahala pekee ambako falsafa ya maisha bora kwa kila Mlibya ilifanikiwa.

Neema zote hizo zililetwa na Gaddafi aliyeiongoza nchi hiyo kwa sura mbili.

Sura mojawapo ilijaa visasi, mauaji, vitisho na ubabe. Yeyote aliyetofautiana naye alikwenda na maji. Hakuwa na mzaha hata kidogo.

Mapambano ya kumwangusha madarakani yalipoanza hadi anauawa adhuhuri ya Oktoba 20, 2011 katika Mji wa Sirte, hakukuwa na sababu maalumu iliyotangazwa ila kuna kijana alisema: “Tunachotaka ni kuishi maisha ya kawaida. Kuwa na uhuru wa mawazo kama vijana wengine duniani.”

Wakati miaka mitano sasa imetimia tangu aanguke, lakini kuna marais wengine wa Afrika wanawaongoza wananchi wao kama Gaddafi. Kutokana na utawala wao, kisa mkasa kinaamini kama Gaddafi ameanguka na wao iko siku wataanguka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles