KALONZO: RAILA ATAKUWA RAIS WA MUHULA MMOJA

0
406

THARAKA NITHI, KENYA


MGOMBEA urais kupitia muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga atahudumu urais kwa muhula mmoja iwapo atashinda, Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amesisitiza.

Kalonzo ambaye ni mgombea mwenza wa Raila, amewahakikishia wafuasi wake kauntini hapa juzi kuwa hakuna mgombea mwingine wa upinzani atakayepingana naye katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Akizungumza kwa lugha ya Kikamba, makamu huyo wa zamani wa rais alisema. “Bila kuficha chochote kwenu, Raila Odinga atashikilia kiti cha urais kwa muhula mmoja wa miaka mitano kama tulivyokubaliana kimaandishi, si kama makubaliano ya nyuma yasiyo rasmi.

“Sasa ni wazi tumekubaliana Raila atasaidia kuihamisha Kenya katika kiwango kingine cha mafanikio na mwaka 2022 atakuwa Kalonzo Musyoka mwenye jukumu hilo. Hakuna lingine,” alisisitiza.

Kiongozi huyo wa Wiper alisema upinzani unaelekea kupata ushindi dhidi ya Jubilee na alikituhumu chama tawala kwa njama za kuleta wasiwasi wa kisiasa katika ngome za NASA.

“Tunawahimiza wafuasi wetu kuwa macho na kulinda katika vituo vya kura kwa sababu tuna taarifa Jubilee imekula njama za kuwatisha wapiga kura kutoka jamii fulani waliopo katika miji mikubwa,” Kalonzo alisema na kuongeza kuwa kila Mkenya ana haki ya kupiga kura.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here