30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

KALONZO MUSYOKA: UAMUZI WA MOI ULIVYOIPOTEZA KANU KISIASA 2002(4)

KALONZO MUSYOKAMAKAMU wa Rais wa zamani wa Kenya, ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka, amezindua kitabu chake kipya Jumatano wiki nne zilizopita.

Kitabu hicho kiitwacho ‘Against All Odds’, kinaelezea safari yake inayoanzia eneo la Tseikuru huko Kitui, Ukambani alikozaliwa na kukulia wakati wa Vita za Mau Mau na Shifta hadi kufikia wadhifa wa pili kwa ukubwa nchini humo na namna alivyoshindwa kufikia ndoto zake za urais miaka ya 2002, 2007 na 2013.

Kwa leo kama ilivyotafsiriwa na mwandishi wetu, baada ya matoleo matatu yaliyopita kujikita namna alivyouona uhusiano wake na Raila Odinga, leo maelezo yake yanaangazia uamuzi wa Rais Daniel Arap Moi kumteua mwanasiasa mchanga Uhuru Kenyatta kukiwakilisha Chama cha KANU katika uchaguzi wa urais mwaka 2002. Uamuzi huo ulikipoteza katika ramani ya siasa chama hicho kilichoasisi uhuru wa Kenya. Sasa endelea…

Kufikia chaguzi za mwaka 1997, nilikuwa tayari natosha kuwania urais, ila kikwazo pekee kilikuwa Rais Moi alikuwa bado katika mchuano huo.

Moi alikuwa kama baba kwangu na hivyo nisingeweza kuwania urais dhidi yake.

Lakini wakati enzi hizo za Moi zikielekea kukoma mwaka 2002, shinikizo kutoka kwa marafiki, wapiga kura na vyombo vya habari kunitaka kugombea urais lilipamba moto.

“Je, atawania tena urais?” ni swali moja fupi lililokuwa likisumbua wengi ndani ya KANU.

Ikichochewa na dhamira yangu, nilimwendea Moi.

Nilitaka kujua iwapo angeruhusu Kanu kuchagua mpeperusha bendera wake kwa njia ya demokrasia.

Moi hakujibu mara moja swali hilo, lakini wiki chache baadaye kwa mshangao wa wengi alitangaza kuweka majeshi yake nyuma kwa Uhuru Kenyatta, akivitosa vigogo lukuki.

Kitendo hicho cha Moi kilisababisha uasi ndani ya chama na hivyo kutishia kukisambaratisha.

Na juhudi za Moi za kuleta maridhiano kati ya waasi wa chama cha Kanu na Rais Uhuru Kenyatta aliyemteua kuwa mrithi wake ziligonga mwamba kwenye mikutano kadhaa ikiwamo Ikulu.

Kiongozi huyu wa Wiper, anasema kulikuwa na mlolongo wa mikutano katika Ikulu, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002, ambao kama ilivyotabiriwa kutokana na kuweka mwanasiasa mchanga, Chama cha Kanu kilishindwa na muungano wa Narc kwenye uchaguzi huo.

Na hadi sasa KANU inajaribu kufurukuta kisiasa bila mafanikio.

Kwa mujibu wa Musyoka katika mkutano wa Ikulu uliofanyika  Oktoba 10, 2002 ulihudhuriwa kinara wa Cord Raila Odinga, marehemu Prof George Saitoti, Moody Awori, Nicholas Biwott na Yusuf Haji.

Viongozi hao walimkabili Moi na kumwambia wazi kwamba Kanu ingeshindwa vibaya kwenye uchaguzi huo ikiwa angebadili uamuzi wake huo.

Hata hivyo, Moi aliwajibu kwa kuwaambia kwamba walikuwa wakimpinga yeye, si uamuzi wake wa kumteua Uhuru.

“Hampingi chaguo langu (Uhuru) ila mimi,” akasema Moi.

Hata hivyo, Musyoka akamjibu Moi: “Ikiwa ni hivyo Mzee nakuomba kwa heshima na kwa niaba yetu sote pamoja na chama ujiondoe katika mchakato huu.”

“Itakuwa vyema kuwashirikisha wajumbe wa chama kumchagua kidemokrasia mtu wanayeona anafaa kuwania urais kwenye Uwanja wa Michezo wa Kasarani badala ya kuwachagulia.”

Kauli hiyo yenye ukweli ilikuwa chungu kwake na hivyo haikumfurahisha na ikaashiria mwisho wa mkutano huo.

Mkutano huo ulifanyika kipindi chama hicho kikiwa katika matayarisho ya kongamano la wajumbe ambapo Kenyatta alipitishwa kuwania urais.

Musyoka anasema kuwa huo ndio ulikuwa mkutano wa mwisho kati yao na Moi.

Kutoka hapo, viongozi waasi walifahamu kwamba walikuwa kivyao.

“Genge la Moi ndani ya KANU lilikuwa limeanza kubadilisha majina ya wajumbe, hata wilaya tunazotaka. Tulijua kwamba hilo lilikuwa na maana ya kujiandaa kutufurusha chamani,”anasema.

Baada ya mkutano huo wa Ikulu, viongozi waasi walielekea katika Mgahawa wa Serena ambapo waliwahutubia wanahabari kuhusu msimamo wao.

“Tulihofu kuwa Kitengo cha Habari cha Rais (PPS) kupitia mkuu wake Lee Njiru, kinaweza kutangaza kwa Wakenya wote kuwa tumebadilisha msimamo wetu na kuunga mkono chaguo la Uhuru kuwania urais,” anasema kwenye kitabu chake hicho.

Odinga, aliyekuwa akielekea mazishini katika eneo la Nyanza, hakuwa kwenye kikao hicho na alieleza msimamo wao katika mazishi hayo.

Musyoka pia anaeleza kuhusu yaliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi na nyumbani kwa Moi, Kabarak, Nakuru na kwamba Moi alipenda kufanya mikutano na wazee kutoka jamii mbalimbali mjini Nairobi.

“Mikutano hiyo ilifanyika nyumbani kwake Kabarak. Kwanza, aliwaita wazee kutoka jamii ya Waluo ili kukutana na wenzao kutoka jamii ya Wakalenjin.

Baadaye alikutana na wazee kutoka jamii ya Abaluhya. Ujumbe mwingine ulijumuisha wazee kutoka jamii ya Akamba, wakiongozwa na marehemu Mulu Mutisya.

Moi alinialika katika mikutano hiyo yote. Angewaalika washirika wake wa karibu, kama marehemu Dk. Bonaya Godana.

Lakini cha kushangaza hakumwalika Uhuru Kenyatta katika mkutano hata mmoja niliyohudhuria.

Na kinyume cha madai yake, Wazee wa Wakalenjin walilalamikia hatua ya Moi kumteua mrithi kutoka jamii ya Agikuyu,” anasema.

Wakati wa mkutano na wazee kutoka jamii ya Abaluhya, JD Otiende, ambaye alihudumu katika baraza la kwanza la mawaziri baada ya Kenya kupata uhuru ndiye aliongoza mazungumzo hayo.

“Walidhani kwamba mwanao, Musalia Mudavadi, ndiye angemrithi Moi. Hata hivyo, walifeli. Mambo yalikuwa kinyume, kwani badala yake, Mudavadi alipewa nafasi ya Makamu wa Rais katika muda usiofaa kwa safari yake ya kisiasa,” Musyoka anaeleza.

“Nilirudi Kabarak nikiwa na ujumbe kutoka jamii ya Akamba. Tulidhani mambo yangenyooka. Tulikubaliana kwamba kamati ndogo kutoka wazee wa Akamba na Wakalenjin ingekutana,” anasema.

Hata hivyo, Moi alionekana kukiuka matarajio ya wote, alipomtangaza rasmi Uhuru kama mrithi wake.

Musyoka anaeleza kwamba kuelekea mwishoni mwa 2001 walifahamu fika  Moi angemteua Uhuru.

Alisema: “Alitarajiwa kutoa tangazo hilo baada ya ziara ya kikazi nchini  Namibia. Hata hivyo, nafikiri kwamba baadhi ya watu wenye ushawishi walimshauri kulichelewesha kidogo suala hilo.

Nadhani watu kama Biwott na Raila, ambaye wakati huo alishirikiana na Moi maana awali walikuwa maadui wakubwa kisiasa, walimtahadharisha.

Lakini Juni 30, 2002, Moi alitoa tangazo hilo akiwa katika eneo la Mlima Elgon, hali iliyoonekana kumsononesha Mudavadi.”

Musyoka anasema kuwa baada ya tangazo hilo, aliagizwa kufika katika Ikulu, alikofahamishwa kuwa tangazo hilo halingebadilishwa. Na juhudi za Mutisya kuonana na Moi ziligonga mwamba.

Katika mojawapo ya mikutano hiyo, Musyoka asema kuwa Moi alimwambia kwamba alikuwa ashaamua ni nani angemrithi.

Awali hilo lilipobainika nilirudi jimboni kwangu kwenda kutuliza akili na niliporudi, Moi aliniita Ikulu.

Nilienda ofisini kwake na akaniambia:  “Unajua Stephen, nimefikiria sana kuhusu suala hili. Usijisumbue kumleta Mzee Mulu Mutisya ama wazee wa Akamba kukutana na wazee wa jamii ya Kalenjini, kwa sababu wazee wa Wakalenjin wameshaamua kumuunga mkono Uhuru Kenyatta.” .

Nilivunjika moyo na sikujibu chochote. Aliniambia niende na kumjulisha Mulu kuhusu uamuzi wake.

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles