31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kalonzo atikiswa ndani ya chama chake

Na Isiji Dominic

ALIYEKUWA Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka, kwa siku za hivi karibuni amejikuta katika wakati mgumu kutoka kwa baadhi ya wanachama wa chama chake cha Wiper huku magavana watatu wakiungana kumtaka akae pembeni.

Chama cha Wiper ni moja ya vyama vinne vikubwa vya siasa vilivyoungana kuunda Muungano wa NASA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017 na kumteua Raila Odinga kutoka Chama cha ODM kuwania urais na Kalonzo kuwa mgombea mwenza.

Umaarufu wa Wiper upo Mkoa wa Mashariki na wafuasi wake wengi ni kutoka jamii ya Wakamba. Wao wanamuona Kalonzo kama chaguo lao la Rais wa Kenya ukizingatia alishawahi kuwa Makamu wa Rais katika Serikali ya Mseto chini ya Rais Mwai Kibaki baada ya machafuko ya kisiasa yaliyotokea kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Hata hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2013, Kalonzo aliweka pembeni azma yake ya kugombea urais na kumuunga mkono Raila na akafanya vivyo hivyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi. Kufuatia Rais Uhuru Kenyatta na Raila kuzika tofauti zao za kisiasa na kuamua kufanya kazi kwa pamoja, Kalonzo naye alisema atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru.

Kauli hiyo iliwaghadhabisha baadhi ya viongozi na wanachama wa Wiper ambao waliona kitendo cha Raila kufanya kazi na Rais Uhuru ni fursa pekee ya yeye (Kalonzo) kujiimarisha kama kiongozi mkuu wa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Tayari magavana watatu Dk. Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) waliungana na kusema jamii ya Wakamba inahitaji uongozi mpya unaolenga maendeleo.

“Kwa nia ya kusonga mbele, tutazungumza kwa lugha moja tuunganishe jamii na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali kuu kuhusu masuala yanayogusa watu wa kwetu,” alisema Dk. Mutua.

Ukaribu wa Profesa Kibwana ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha Wiper na kiongozi wa chama hicho, Kalonzo, unazidi kudorora na mwishoni mwa wiki iliyopita kulivuma taarifa ya mwenyekiti huyo kuandika barua ya kujiuzulu.

“Unapokuwa kwenye ndoa na unajaribu kila njia kulinda ndoa ili isivunjike lakini mambo hayaendi sawa, unafanya nini?” Profesa Kibwana aliwauliza wananchi aliokuwa anawahutubia ambao wote kwa pamoja walisema njia sahihi ni kuachana na ndoa hiyo.

“Katika tamaduni za Wakamba, wakati mwanamke anaolewa, wazazi wake wanapewa mbuzi watatu lakini wakitengana mbuzi hao wanarudishwa. Sasa kwa sababu nyinyi ndiyo mlionipa mbuzi, nimezirudisha na sina nia tena ya kuendelea na ndoa hii, nimeondoka,” alisema.

Profesa Kibwana alimshutumu Kalonzo akisema anatumia wanachama wadogo kupambana naye ndani ya Wiper akisisitiza ameua demokrasia ndani ya chama kwa kutoruhusu mtu kuhoji maamuzi yake.

Mshirika wa karibu wa Kalonzo ambaye pia ni Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka, amemtaka makamu rais huyo wa zamani kustaafu siasa kwa kile alichodai hana mawazo mapya.

“Lazima tueleweke tunaposema imefika muda Kalonzo kustaafu siasa na kuruhusu kizazi kipya cha uongozi kushika hatamu,” alisema mbunge huyo na kuongeza jamii yao haiwezi kuendelea kuwekeza kisiasa kwa Kalonzo katika azma yake ya kuwa rais na kutarajia mabadiliko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles