24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Kalemani: Tanesco kateni umeme kwa wadaiwa sugu

 MWANDISHI WETU– DODOMA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme nchini( TANESCO) kuendelea kukata umeme kwa wadaiwa sugu ili kukusanya mapato zaidi na kulipa madeni ya shirika hilo.

Dk. Kalemani alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, alipokutana na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco, kuzungumzia tathimini ya miaka mitano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kutuo cha kupoza na kuzambaza umeme cha Zuzu. 

Katika kikao hicho, mambo mbalimbali yalijadiliwa kuhusiana na nishati ya umeme inayozalishwa nchini kwa lengo la kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi kwa nchi, Shirika na watumiaji wa umeme huo ikiwemo viwanda, wafanyabiashara na matumizi mengine.

Dk. Kalemani aliiagiza Tanesco, kulipa madeni yote inayodaiwa na kutoongeza madeni mapya, vilevile wadaiwa sugu wakumbushwe madeni yao,na endapo hatawalipa, Tanesco iwakatie umeme, kwa kufanya hivyo kutamaliza tatizo la wadaiwa sugu. 

“Tanesco inadaiwa madeni makubwa, pia ina wateja wengi sana ambao ni wadaiwa sugu wanaodaiwa fedha nyingi sana na hawalipi ,zimo Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi, pamoja na watumiaji wa kawaida, ninawaagiza nendeni mkawakatie umeme! narudia tena mkakate umeme! mkishaukata, wahusika watalipa na wataonyesha ushirikiano mkubwa, tofauti na kumdai kawaida tu,” alisema Dk. Kalemani. Kuhusu wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme, Dk. Kalemani, aliitaka Tanesco, bodi na watendaji wa Wizara ya Nishati, kushirikiana kwa pamoja kutafuta njia sahihi naya kisasa zaidi ya kubaini wizi wa umeme,unaofanywa na watu wasiowaaminifu na kusababisha hasara kwa shirika na kupoteza mapato ya taifa.

“Wizi wa umeme upo na haukubaliki, tuweke mfumo sahihi wa kisasa kubaini wahusika, tuache na hii tabia ya kukimbizana kimbizana na wezi, pia sisi watumishi tuwe wazalendo,na wasimamizi wazuri wa miundombinu yetu,vilevile tuwe na walinzi wenye weledi katika miradi yetu bila kujali niya serikali au mtu binafsi, jukumu la ulinzi ni letu sote faida ya Taifa kwa jumla,” alisema 

Aidha aliwataka kuendelea kufanya tathmini na uwiano wa gharama za kutengeneza nguzo za Zege na nguzo zinazotumika sasa, ili kuangalia uwezekano wa kutumia nguzo za zege katika maeneo yote nchini lakini kwa gharama nafuu, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kuoza ama kuungua kwa nguzo katika maeneo mbalimbali.

 Hata hivyo aliweka wazi kuwa katika baadhi ya maeneo machache ambayo ni korofi nguzo za zege zimeanza kutumika japo ni za gharama kubwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka Tanesco kuangalia uwezekano wa kutoa zawadi kubwa kwa wasamaria wema wanaotoa taarifa za siri kuhusu wanaohujumu na kuiba umeme tofauti na ile inayotolewa sasa, ambayo pia huchukuwa muda mrefu kuikabidhi kwa mhusika.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles