32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kalemani aomba bajeti ya trilioni 2.142/- miradi ya umeme, gesi

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amewasilisha bajeti yake na kuomba bajeti ya Sh trilioni 2.142 kutekeleza miradi mitatu ya kimkakati katika mwaka wa fedha 2019/20.

Akiwasilisha bajeti hiyo jana bungeni jijini hapa, Dk. Kalemani aliitaja miradi hiyo ni ya uzalishaji umeme ya maporomoko ya Mto Rufiji megawati 2,115 ambao unagharimu Sh trilioni 1.44, mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu (REA) Sh bilioni 363.11 pamoja na mradi wa kusambaza umeme wa Kinyerezi I Extension megawati 185 wa Sh bilioni 60.

Alisema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya nishati nchini tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ni kuliwezesha taifa kutokuwa na mgawo wa umeme katika kipindi chote cha utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/19.

Dk. Kalemani alisema lengo la Serikali ni kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

“Miradi mingine ni wa maporomoko ya Rusumo utakaozalisha megawati 80, Ruhudji megawati 358,  Rumakali megawati 222 pamoja na kuimarisha mifumo ya uzalishaji umeme nchini,” alisema.

Alisema mifumo itaboreshwa kupitia mradi wa North-West Grid Extension wa kilovoti 400 yenye umbali wa kilometa 1,384 iliyojumuisha Iringa, Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma hadi Nyakanazi.

Pia utahusisha Singida, Arusha hadi Namanga kwa kilovoti 400 kwa kutumia kilometa 414, Rufiji, Chalinze, Dodoma (Kv 400) wa kilometa 512, Rusumo, Nyakanazi (Kv 220) utakaohusisha kilometa 98 na Geita, Nyakanazi (Kv 220) utakaohusisha kilometa 133.

Alisema mradi huo pia utapita Tabora, Urambo, Kaliua, Nguruka hadi Kidahwe mkoani Kigoma (Kv 132) utakaohusisha kilometa 319 na Tabora, Ipole Inyonga hadi Nsimbo mkoani Katavi (Kv 123) kwa kujumuisha kilometa 381.

“Kuendelea na kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, kuimarisha shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia, kuongeza kasi ya usambazaji gesi asilia na kuendeleza miradi ya nishati jadidifu,” alisema.

Akizungumzia hali ya upatikaji umeme, Dk. Kalemani  alisema kuwa hali ya upatikanaji umeme imeendelea kuimarika katika kipindi chote cha bajeti ya mwaka 2018/19.

Alisema mahitaji ya umeme yameongezeka kutokana na kuongezeka shughuli za kiuchumi zenye kuhitaji nishati ya umeme wa kutosha.

“Kati ya jumla ya megawati 1,601.90 zilizopo nchini, megawati 1,565.72 zimeunganishwa katika mfumo wa gridi ya taifa na megawati 36.18 zipo nje ya mfumo wa gridi ya taifa,” alisema.

Akizungumzia kuhusu nishati ya gesi asilia na mafuta, Dk. Kalemani alisema hadi kufikia Mei mwaka huu, futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia zimegunduliwa nchini.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018/19, shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia zimeendelea kutekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni za kimataifa za mafuta (IOCs).

“Uchukuaji wa data za mitetemo za 2D zenye kilometa 442 za mstari katika kitalu cha Ruvu umekamilika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles