Kalemani aipa kibarua Tanesco Singida

0
1264

 MWANDISHI WETU – SINGIDA 

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mkoa wa Singida kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanaweka umeme kwenye vijiji 11 vilivyopo Jimbo la Singida Mashariki. 

Aidha ameiagiza Tanesco Singida kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi aanze kusimika nguzo mapema katika Tarafa ya Mungaa Lighwa, Ntuntu,Misughaa na Kikio ili umeme uwashwe kwenye Vijiji kabla ya Juni, mwaka huu

Dk. Kalemani alitoa maagizo hayo jana wilayani Ikungi akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya umeme ambapo amewasha umeme katika vijiji viwili vya Matare na Nkuhi. 

“Nampongeza sana Mbunge wenu Miraji Mtaturu, kwani anafuatilia sana miradi ya wananchi wake, tangu amechaguliwa na kuapishwa ni miezi mitano tu lakini mnaona mambo yalivyo, tumewasha vijiji viwili je angekaa miaka minne hali ingekuwaje?,” alihoji Dk. Kalemani. 

Akizungumzia ugonjwa wa corona, alisema kuwa isiwe sababu ay kusimama kwa kazi ya miradi ya umeme nchini. 

 “Ndugu zangu ugonjwa huu wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID 19) usikwamishe kazi za kuunganishia umeme wananchi ila mfanye kazi kwa tahadhari,tutaendelea kukagua miradi ya umeme kila mahali kwa kuwa wananchi wanahitaji umeme na Rais Dk. John Magufuli ameidhinisha Shilingi bilion 40 kwa Mkoa wa Singida ili kutekeleza miradi hii hivyo ni lazima tuisimamie,” alisema Dk. Kalemani. 

Pamoja na hayo Dk. Kalemani amesisitiza wananchi kutolipishwa nguzo na gharama za kuunganishiwa umeme amesema ni Sh 27,000 na sio vinginevyo. 

“Katika hili niagize hapa mkandarasi wa Cyba Contractors Ltd ya Jiji Mbeya aliyelalamikiwa kuwatapeli wananchi baada ya kuchukua pesa zao na hajafanya wiring mpaka sasa atafutwe,” alisema 

Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo alisema katika kata 28 zilizopo wilayani humo ni kata 18 tu ndio zimefikiwa na umeme hivyo kumuomba waziri aendelee kuwasaidia. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here