NA MOHAMED KASSARA
-DAR ES SALAAM
NI rasmi kipa mahiri nchini , Beno Kakolanya atavaa jezi zenye rangi nyekundu na nyeupe kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba.
Kipa huyo amejiunga na Wekundu hao,
baada ya
kuichezea Yanga kwa misimu minne, akitokea kikosi cha Maafande wa Jeshi
la Magereza,Tanzania Prisons ya Mbeya.
Mwishoni mwa mwaka jana, Kakolanya aliomba kuvunja mkataba na Yanga, kutokana na kile alichodai klabu hiyo ilishindwa kumlipa shahiki zake, lakini hata alipopata ufumbuzi wa madai yake hakuweza kurejea katika kikosi hicho cha Jangwani, baada ya kuwekewa ngumu na kocha Mwinyi Zahera aliyedai kipa huyo ni mtovu wa nidhamu.
Kusajiliwa kwake Simba, kumekamilisha tetesi za muda mrefu za kutakiwa na klabu hiyo ya Msimbazi, ambayo jana kupitia akaunti rasmi iliachia picha ya kipa huyo akisaini mkataba, akiwa na meneja wake, Selemani Haroub.
Horoub pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba.
Usajili wa Kakolanya unafanya idadi ya wachezaji ambao mpaka sasa wamethibitika kumwaga wingo wa kuichezea Simba msimu ujao kuwa watano.
Wengine ni kipa Aishi Manula, John Bocco, Jonas Mkude na Erasto Nyoni ambao wameongeza mikataba ya miaka miwili miwili, baada ya awali kuelekea ukingoni.
Kakolanya ni wazi atalazimika kupambana kweli kweli ili kupata nafasi ya kukaa langoni, kutokana na kukabiliwa na ushindani wa Manula ambaye amekuwa akitumika kipa wa kwanza, akisaidiana na Deogratius Munishi ‘Dida’.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kakolanya alisema amesaini Simba ili kupata ushindani ambao hakuwa anaupata kipindi akiwa Yanga.
“ Najua kuna ushindani wa namba na inaweza kuwa vigumu kumweka benchi Manula (Aishi), lakini nini naenda kufanya.
“ Yanga nilikuwa namba moja, sikuwa napata ushindani kitu ambacho kilinifanya nijione mimi ni bora, lakini uwepo wa Manula Simba utanifanya niamini nitakuwa bora zaidi kwa kuwa nitalazimika kupambana zaidi ili nipate nafasi ya kucheza ,”alisema Kakolanya.
Mbali na Kakolanya, taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, zinaeleza kuwa aliyekuwa nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajib , pia amesaini kuichezea timu hiyo msimu ujao, ingawa hakuna uthibitisho uliotolewa na klabu hiyo.
Wengine wanaotajwa sana ni pamoja na straika wa Nkana ya Zambia,Walter Bwalya, ambaye yuko nchini tayari tangu juzi.
Pia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ni kati ya walioongeza mkataba, huku Emmanuel Okwi akiwa mbioni kufanya hivyo.
Mtendaji wa Mkuu wa Simba (CEO),Crescentius Magori, alisema, huo ni muendelezo wao wa kutambulisha wachezaji watakaoichezea timu hiyo msimu ujao.
“ Jana (juzi)nilisema katika mkutano wangu na vyombo vya habari kuwa tumeshakamilisha usajili wetu kwa zaidi ya asilimi 90, ikiwemo kuwaongeza mikataba wachezaji wetu muhimu ambao kocha anawahitaji.
“Usajili huu unalenga zaidi mashindano ya kimataifa yaliopo mbele yetu na ndio maana kila nafasi tunakuwa na wachezaji zaidi ya wawili.
“ Kila siku tutakuja na mtu mwingine, Wanasimba wasiwe na shaka tunafanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kufuata matakwa ya kocha wetu ambaye ndiye mwenye jukumu la kuipa matokeo chanya timu,” alisema Magori.