SAO PAULO, BRAZIL
NYOTA wa zamani wa klabu ya Real Madrid na AC Milan, Ricardo dos Santos ‘Kaka’, ametangaza rasmi kustaafu soka huku akiwa na umri wa miaka 35.
Mchezaji huyo ambaye alikuwa anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, amestaafu soka akiwa anaitumikia klabu ya Sao Paulo ya nchini Brazili, ambapo alikuwa anacheza kwa mkopo akitokea klabu ya Orland City inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani.
Nyota huyo wa Brazili mara ya mwisho kucheza soka katika klabu yake ilikuwa Oktoba mwaka huu, huku timu yao ikikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Colombus Crew, hivyo aliamua kuweka wazi kuwa muda wake umefika wa kustaafu soka.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Kaka aliamua kuwaaga mashabiki zake huku akisema ni maamuzi sahihi kwa upande wake.
“Baba, ninaweza kusema maisha yangu sasa ni zaidi ya vile ambavyo nilikuwa nafikiria, naomba maisha yangu yawe chini ya Yesu.
“Nakushukuru sana kwa kunifanya niwe hapa, safari yangu ilikuwa ndefu na sasa nipo tayari kwa safari nyingine ya maisha yangu. Kwa jina la Yesu. Amen,” aliandika Kaka.
Mchezaji huyo alianza kuonesha ubora wake kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2002 ambapo walifanikiwa kulitwaa akiwa na kikosi chake cha Brazili, baada ya hapo klabu mbalimbali barani Ulaya zikawa zinagombania saini yake kuanzia mwaka 2003 AC Milan walifanikiwa kumsajili nyota huyo.
Mbali na kutwaa Kombe la Dunia, lakini alifanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu nchini Italia msimu wa 2003/2004, Italian Super Cup 2004/05, Confederations Cup 2005 na 2009, Ligi ya Mabingwa 2006/07, UEFA Super Cup 2007/08, Spanish Cup 2010/11, Ligi Kuu Hispania, 2011/12.
Amewahi kuchukua tuzo mbalimbali ikiwa pamoja na mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu wa 2006/07, mchezaji bora wa mwaka nchini Italia, 2004 na 2007, mchezaji bora wa mwaka barani Ulaya wa UEFA 2007 na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA Ballon d’Or 2007.
Mchezaji huyo aliongeza kwa kusema lengo la kustaafu soka ni kuwapisha vijana wenye damu changa waweze kutumia nafasi hiyo na kuonesha vipaji vyao kwa ajili ya kupigania Taifa pamoja na klabu zao kwenye michuano mbalimbali duniani.