Na Asha Bani, Mtanzania Digital
Walimu wametakiwa kuchukua hatua za makusudi na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa watoto mashuleni wanapata elimu kuhusu ukatili ili waweze kujilinda wakiwa shuleni na nyumbani.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki katika kongamano la walimu lililofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa kufungua rasmi kongamano hilo, Kairuki alibainisha kuwa walimu wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wana uelewa wa aina za ukatili, mbinu zinazoweza kutumika katika kujilinda dhidi ya ukatili na hatua za kuchukua ili kuripoti matukio hayo pindi yanapojitokeza.
“Mbali na kuelimisha wanafunzi kuhusu ukatili, nawaasa walimu kuendelea kutoa ushirikiano kwa wazazi na wadau wengine katika mikakati mbalimbali ya kupambana na ukatili,” amesema Kairuki.
Naye muandaaji wa Kongamano hilo ambaye ni Muasisi na Mkurugenzi wa shule za Rightway, Mercy Mchechu alitoa wito kwa walimu kulinda watoto walio mikononi mwao ili kunusuru kizazi.
“Ametokea mwalimu mwingine aitwae mitandao ya kijamii, naye amekuwa na nguvu kubwa kuliko sisi. Changamoto za ukatili zinazowakabili watoto ambazo zinachangiwa na mifumo ya malezi zinaweza kurekebishika, ila tu zinahitaji mbinu na mikakati, hivyo walimu tushirikiane kwa pamoja na wazazi na wadau katika kulinda watoto,” amesema.
Jessica Kusikula ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kantui kutoka wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Ameshiriki kongamano hilo akiwa na walimu wenzake kumi kutoka wilaya mbalimbali mkoani humo. Jessica ameelezea mtazamo wake kuhusu kongamano hilo kwa kusema:
“Nina furaha kushiriki kwenye kongamano hili na natarajia kuondoka hapa na elimu ambayo itanisaidia kuwaelimisha wengine katika jamii kuhusu ukatili dhidi ya watoto mashuleni na majumbani,” amesema.
Kongamano hilo la siku moja limefanyika katika ukumbi wa Oasis Village ulioko Mbezi Beach Beach jijini Dar es Salaam na kukutanisha walimu takribani mia tano kutoka mikoa mbalimbali Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Zanzibar na mingineyo.