33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki akonga wabunge sekta ya uwekezaji

MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Agellah Kairuki, amewaeleza wabunge kwa undani utekelezaji wa ajenda ya taifa ya uwekezaji na kusema  kwamba kutokana na uzoefu uliopatikana, sheria ya mpya za uwekezaji, uboreshaji wa mazingira ya biashara na uvuvi zinaandaliwa na Serikali.

Akijibu maswali na michango ya wabunge wa kamati 12 za kudumu za Bunge waliokutana naye jijini hapa juzi, Kairuki alisema sheria mpya zinaandaliwa kusawazisha mapungufu yaliyojitokeza na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana.

“Mafanikio yetu katika kutekeleza agenda ya taifa ya uwekezaji ni makubwa na yako wazi. Lakini tumejifunza mambo mengi, tumekutana na changamoto pia. Tanakuja na sheria mpya ili tuwe na mifumo iliyo bora zaidi… miswada hiyo tukiileta mbele yenu tunaomba ushirikiano wenu,” alisema Kairuki.

Aliitaja sheria hiyo kuwa ni ya uwekezaji na sheria ya kuboresha mazingira ya biashara (Business Facilitation Act).

Akijibu swali, Kairuki amewahakikisha wabunge kwamba hakuna taasisi  maalumu duniani inayotoa taarifa kuhusu uwekezaji katika nchi za dunia, na kufafanua kwamba hata hivyo zipo taasisi zinazofuatilia mienendo ya uwekezaji duniani.

Alisema kwamba Tanzania siyo kisiwa, na kwa hiyo inaangalia mifumo, matatizo, changamoto na mafanikio ya  nchi nyingine, hasa Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Hata hivyo Serikali imeagizwa kuchukua hatua za kunusuru mkwamo wa uratibu wa uwekezaji wa viwanda kati ya sekta ya umma na binafsi katika ngazi ya mikoa na wilaya nchini, kwa kuongeza vituo vya pamoja vya usimamizi na uratibu kwenye maeneo mbalimbali ya kimkakati.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema kamati hiyo inashauri Serikali ihakikishe inaongeza vituo vya pamoja vya usimamizi na uratibu ili kuwezesha taasisi zote husika kuratibu kwa pamoja masuala ya uwekezaji kwa urahisi zaidi na kupunguza urasimu usio wa lazima, ambao unaweza kukatisha tamaa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema kwa kuwa imebainika kuwepo kwa mikoa na wilaya iliyoshindwa kuratibu ipasavyo sekta ya umma na sekta binafsi, na kwa kuwa imeshindwa kuratibu majadiliano ya masuala ya biashara na uwekezaji, inachelewesha na kukwamisha jitihada za Serikali katika kuchochea uwekezaji wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Hivyo basi kamati inashauri Serikali kuanza kutekeleza mwongozo wa majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika ngazi ya mikoa na wilaya ili kutatua changamoto hiyo na kuchochea uwekezaji katika ngazi za mikoa na wilaya nchini,” alisema Mchengerwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles