30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki ahamasisha kilimo cha pamoja

MWANDISHI WETU -KILIMANJARO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki, ameutaka uongozi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuhamasisha wananchi kulima kilimo cha pamoja, hususani mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuwezesha kilimo chenye tija na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Rai hiyo aliitoa jana katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Alisema kilimo cha pamoja kina manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwa wawekezaji wataweza kununua mazao mengi kwa pamoja, na hivyo kuinua uchumi.

Kairuki alisema yapo mazao yenye uhitaji mkubwa katika viwanda mbalimbali nchini, akitolea mfano wa zao la mtama ambalo alisema kiwanda kimojawapo cha KBL kilichopo wilayani Mwanga kina mahitaji ya zaidi ya tani 6,000 hivyo ni dhahiri kuwa soko la uhakika litapatikana endapo wakulima watalima kilimo cha pamoja na kuzalisha zao hilo kwa wingi.

“Wilaya ya Same ina fursa nyingi za kilimo kutokana na ardhi yake kuweza kustawisha mazao ya aina nyingi tofauti na maeneo mengine, kwani yapo maeneo ya umwagiliaji ambapo wanaweza kulima kilimo cha umwagiliaji na maeneo mengine makubwa ya kilimo kingine, hivyo hamasisheni kilimo cha pamoja chenye tija,” alisema Kairuki.

Aidha aliutaka pia uongozi wa wilaya hiyo kushughulikia migogoro ya ardhi hususani inayohusu wananchi na wawekezaji kwa haraka, ili kuweza kutoa mwafaka na kuwezesha uwekezaji kuendelea kwa tija.

“Mwekezaji anapofika mahali akakutana na migogoro, inamchelewesha kuanza kazi zake, lakini pia inakwamisha kasi ya uwekezaji, hivyo hakikisheni mnashughulikia migogoro kwa haraka iwezekanavyo ili kupanua wigo wa uwekezaji,” alisema Kairuki.

Katika hatua nyingine, Kairuki alitaka kuangaliwa uwezekano wa kuanzishwa kwa machinjio ya kisasa katika wilaya hiyo, akieleza kuwa ipo mifugo mingi hivyo itakuwa fursa nzuri ya uwekezaji.

“Suala la kuanzisha machinjio liende sambamba na upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa machinjio ili kuwawezesha kuitumia na kuleta tija kwa wilaya,” alisema Kairuki.

Mbali na hilo, alitaka pia wilaya hiyo  kujenga makumbusho ya madini, ambayo watalii pamoja na wananchi watatembelea na kujionea madini mbalimbali ambayo yanapatikana wilayani humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule alisema wakulima kulima zao moja katika eneo moja itawarahisishia wanunuzi kupata mazao wanayohitaji kwa wingi, na hivyo kuwa na masoko ya uhakika.

“Wakulima wanapolima mmoja mmoja  au mazao ya aina tofauti katika eneo moja, hayana tija kwao wenyewe na pia kwa Serikali pindi inapotarajia kuuza zao moja kwa wingi kwa wakati mmoja.

“Lakini inapotokea tukasema kata fulani ni ya zao fulani, wanaweza kukusanya mazao yakauzwa kwa pamoja na kuleta tija,” alisema Senyamule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles