23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kailima awataka Nida kutunza siri, kuwajibika

Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kufanya kazi kwa kushirikiana, uwajibikaji na kutunza siri za ofisi kwa mujibu wa sheria.

Hayo aliyasema jana wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi Tawi la Nida.

Kailima alisema mafanikio ya mamlaka hiyo ni pamoja na kushirikiana katika utendaji wa kazi ili kuleta weledi, na pia kuepuka kutoa siri za ofisi kwa mujibu wa utaratibu wa utumishi wa umma.

Pia aliwakumbusha watumishi hao kutoka Makao Makuu ya Nida na ofisi zake za mikoani kuhakikisha uwajibikaji unakuwepo kwa upande wa mwajiri na mwajiriwa kwa kufanyiwa kazi kile kinachotakiwa kufanyiwa kazi na kisichohitajika kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.

“Tukoseane kwa nia ya kuboresha, tusikoseane kwa nia ya kubomoa kwa sababu ya kupata fursa hii ya kuwa na haki na hadhi sawa, na pande zote mbili ziwajibike kuwajibishana,” alisema Kailima.

Alisema watumishi wanapaswa kupewa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka na masuala yanayowahusu kwa utaratibu wa ofisi au unaoidhinishwa na mkurugenzi mkuu na si vinginevyo.

“Muhakikishe mnatoa huduma kwa wananchi sehemu zote nchini kwa weledi, maofisa wafike mapema katika maeneo ya kazi na kutoa vitambulisho vya taifa mapema, na wananchi waridhike na huduma hiyo mnayoitoa, kwa hatua hiyo mtapunguza malalamiko ya wananchi,” alisema Kailima. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Arnold Kihaule alieleza mafanikio ya mamlaka hiyo.

Alisema hadi kufikia Desemba mwaka 2019, wamefanikiwa kusajili wananchi 21,511,321, wageni wakaazi, 19,311 na wakimbizi 274,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

“Pia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imezalisha namba za utambulisho 16,211,654 na kutoa vitambulisho 5,787,869, na vimewafikia wananchi ilipofika mwezi Desemba 2019,” alisema Dk. Kihaule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles