Na WINFRIDA MTOI
-DAR ES SALAAM
BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imekiri kufanya makosa katika uwekaji takwimu na kuitangaza Kagera Sugar kuwa timu iliyoshuka daraja moja kwa moja badala ya Stand United.
Kagera Sugar ilicheza mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Sare hiyo iliifanya ifikishe pointi 44, sawa na Stand United iliyofungwa mabao 2-0 na JKT Tanzania.
Baada ya matokeo hayo, Kampuni ya Azam Media kupitia runinga yake ya Azam yenye dhamana ya kurusha michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ilianika msimamo ukionyesha Stand United imeshuka daraja, lakini ule wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulionyesha Kagera Sugar ndiyo imeaga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura, alisema takwimu za awali zilionyesha Kagera Sugar imemaliza ikiwa nafasi ya 19 na Stand United 18 kutokana na utofauti wa mabao ya kufungwa na kufunga.
Alisema baada ya kufanyiwa marekebisho kwa kupitia tena takwimu, walibaini timu inayostahili kuungana na African Lyon kushuka daraja ni Stand United huku Kagera Sugar ikitakiwa kucheza hatua ya mtoano ‘Play Off’ pamoja na Mwadui FC.
Wambura alifafanua kuwa, licha ya timu hizo kulingana pointi ambazo ni 44, Kagera Sugar ina faida ya tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa ambayo ni hasi 10 wakati Stand United ina hasi 12.
“Katika msimamo wa kwanza hadi kufikia hatua ya kuitangaza Kagera kuwa imeshuka, tuliangalia kanuni, timu zinaanza kutenganishwa kwa pointi, zikilingana zinatenganishwa kwa tofauti ya mabao, zikilingana tunakwenda kwa timu iliyofunga mabao mengi.
“Pia zikilingana hapo inaangaliwa mechi zao mbili walizokutana, nani alipata mabao mengi, zikilingana tunakwenda kuangalia nani alifunga mabao mengi ugenini, zikilingana sehemu zote inabidi zikutanishwe tena kucheza ili kupata wa juu.
“Mkanganyiko uliojitokeza kati ya Kagera Sugar na Stand United, ilikuwa katika utofauti wa mabao, baada ya watu wetu wa data kupitia upya wakabaini kulikuwa na makosa katika kuingiza matokeo ya mechi ya Mei 16, iliyozikutanisha timu hizo,” alisema Wambura.
Alieleza kuwa katika mechi hiyo, Kagera Sugar ilifungwa mabao 3-1, lakini takwimu zilizoingizwa zilikuwa zinaonyesha Kagera ililala mabao 3-0.
Alisema baada ya marekebisho hayo, Kagera Sugar itacheza mechi ya mtoano Juni 2, mwaka huu dhidi ya Pamba FC, kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza na mchezo wa marudiano utakuwa Juni 8, Kaitaba, Kagera.
Kwa upande wa Mwadui FC, watakuwa wageni wa Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita na mechi ya marudiano itachezwa Juni 8, mwaka huu katika Dimba la Mwadui Complex, Shinyanga.