Na Derick Milton, Simiyu
Baada ya Mwaka wa Fedha wa Seriserikali kufungwa Juni 30, 2022, Mkoa wa Simiyu umevunja rekodi ya makusanyo kwa Halmashauri zake kukusanya Sh bilioni 14.2 sawa na asilimia 108.
Kiwango hicho cha makusanyo kinatajwa kuvuka lengo la makusanyo ambalo halmashauri zote sita zilizopo katika mkoa huo zilijiwekea la kukusanya asilimia 100.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Julai 6, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema makusanyo hayo yamevunja rekodi ikilinganishwa na mwaka jana ambapo halmashauri zilikusanya Sh bilioni 10.9 sawa na asilimia 76.
“Katika makusanyo hayo Wilaya ya Maswa ndiyo imekuwa kinara kwa kukusanya asilimia 125, ikifuatiwa na Meatu na Bariadi vijijini zenye asilimia 110 kila moja na zikifuatiwa na Bariadi Mjini yenye asilimia 103 huku Busega ikifunga kwa asilimia 95,” amesema Kafulila..
Kafulila amewapongeza wakurugenzi wote wa Halmashauri hizo kwa kuhakikisha Mkoa unaendelea kuonesha ufanisi katika makusanyo na matumizi huku akiwataka kuendelea kusimamia zaidi ukusanyaji wa mapato.