28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Kafulila: Mfumo kwenye ushirika unawanyonya wakulima

Na Derick Milton, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amesema kuwa mfumo uliopo kwa sasa kwenye Ushirika unawanyonya wakulima badala ya kuwanufaisha kama lengo la kuundwa cha chombo hicho linavyotaka.

Amesema kuwa Taasisi nyingi ambazo zimekuwa zikipata fedha kupitia ushuru wa pamba, zimeshindwa kuwasadia wakulima na badala yake wananufaika viongozi kupitia fedha zinazotokana na pamba ya wakulima.

Amesema kuwa hali hiyo imepelekea wakulima wengi nchini wakiwemo wanaozalisha pamba, kuchukia ushirika licha ya kulazimishwa kupeleka mazao yao Amcos kwa ajili ya kuuzwa kutokana na mfumo uliopo.

Kafulila amesema hayo jana, Alhamisi Novemba 18, wakati kikao chake na viongozi na watalaamu wa vikozi kazi vya zao la pamba kutoka tarafa ya Itilima Wilaya Itilima mkoani humo.

Amesema kuwa Bodi ya pamba, Vyama vya msingi vya Ushirika (Amcos), vyama vikuu vya ushirika, ni vyombo ambavyo vinatakiwa kusimamia zao la pamba na kuwasaidia wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija.

Amesema kuwa vyombo hivyo vimekuwa vikikusanya ushuru unaotokana na zao la pamba ambalo ni jasho la mkulima, na fedha ambazo wanakusanya ni nyingi kila mwaka, lakini wameshindwa kuwasaidia wakulima.

“Kwa mkoa wetu wa Simiyu msimu uliopita Amcos walipata zaidi ya Bilioni 4, Chama kikuu cha ushirika (SIMCU) walipata zaidi ya Milioni 800, Bodi ya pamba nayo ilipata fedha nyingi, lakini fedha hizo hazijarudi kwa wakulima kuwasaidia,” amesema Kafulila.

Aliongeza kuwa msingi wa kuanzishwa kwa vyombo hivyo, ulikuwa kukusanya ushuru na baada ya msimu kuisha basi wanatakiwa kuwasaidia wakulima wakati wa maandalizi ya msimu mpya ili kuweza kuzalisha kwa tija.

“Wengi wamelalamikia huu ushirika, Amcos zinakula pesa, wanaonufaika ni viongozi tu, SIMCU nayo hivyo hivyo na wakulima wengine wanasema hawajawahi kuwaona hata hao SIMCU lakini ushuru wanakata,” alieleza Kafulila.

Alieleza kuwa mfumo mwingine ni jinsi ya wakulima kujiunga katika ushirika, kwani kumekuwepo na masharti magumu kwa wakulima kujiunga lakini katika kuuza pamba au mazao yao wote bila ya kujali kama mwanachama au hapana lazima upeleke Amcos.

“Kama mkoa tumeanza kupambana na hii mifumo kwa kuifanyika marekebisho, tumeanza na hii ya mkulima kuwa mwanachama, tunataka kila mkulima awe mwanachama kwa sharti la kumiliki shamba la pamba,” alisema Kafulila.

Alisema kuwa wamepeleka mapendekezo Wizara ya Kilimo, kubadilishwa kwa masharti ambapo mkulima kigezo cha kujiunga na Amcos kitakuwa shamba lake na siyo vigezo vingine vilivyopo kwa sasa ikiwemo pesa.

Amesema kuwa hali hiyo itafanya wakulima kuongezeka kwenye Amcos na maamuzi kufanywa na wengi, lakini pia kuweza kupata viongozi sahihi na siyo kama ilivyo kwa sasa wanachama ni wachache na wanafanya maamuzi ya wakulima wote.

Hata hivyo Kafulila ameeleza kuwa mbali na hilo kama mkoa watapitia mifumo yote na kuhakikisha inabadilishwa ndani ya mkoa, ambao umejiwekea lengo la kuzalisha tani laki tano katika msimu ujao wa pamba 2021/22.

“Lazima Ushirika urudi kama zamani, siyo kuwanyonya wakulima, lazima urudi katika msingi wake ambao unawataka warudishe fedha wanazopata kwa wakulima, watatue shida za wakulima,” alisema Kafulila.

Baada ya kikao hicho wakulima walimpongeza Mkuu huyo na mkoa, huku wakiunga mkono kufumuliwa na mfumo uliopo kwa sasa ndani ya ushirika kwa kile walichoeleza kuna wizi mwingi.

“Tunamuunga mkono Mkuu wa mkoa, siku nyingi tunalalamikia huu ushirika, umekuwa wa kutunyonya, wakati wa mavuno utawaona lakini wakati wa kulima hawaji kutusaidia,” alisema Minza Sayi Mkulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles