31.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kadogosa awataka wajumbe CCM kutangaza mazuri ya SGR

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kuwa mabalozi wazuri wa kuusemea usafiri wa treni ya SGR.

Hayo yamesemwa leo Januari 16,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, wakati wajumbe hao waliposafiri kwa treni hiyo kuelekea jijini Dodoma kushiriki Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM utakaofanyika Januari 18 na 19 mwaka huu.

Amesema watu 922 wakiwemo wajumbe zaidi ya 600 kutoka Zanzibar, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro pamoja na kundi la wasanii wamesafiri kwa kutumia treni hiyo.

Amesema ujenzi wa reli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM hivyo wajumbe wanapotumia usafiri huo wanajionea kazi ilivyofanyika.

“Kwetu sisi ni heshima kubwa na vilevile ni biashara, wangeweza kuchukua mabasi au hata ndege, tunaowasafirisha ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na ndicho chama kilichounda Serikali ambayo sisi ni watumishi wake.

“Utekelezaji tunaofanya katika shirika letu unatokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM na wanaposafiri watajionea wenyewe utekelezaji wa maono ambayo walikuwa nayo, inawapa nguvu ya kwenda kuzungumza kwa sababu chama lazima kiuzwe na kinauzwa na mafanikio ya yale waliyowaahidi wananchi,” amesema Kadogosa.

Kadogosa amesema wamejipanga kukabili changamoto zozote zitakazojitokeza katika uendeshaji wa usafiri huo na kuwataka Watanzania kuwa walinzi wa miundombinu ya reli hiyo.

Amesema pia wameshashusha mabehewa ya mizigo 264 kati ya 1430 na wanatarajia kuanza kuyafanyia majaribio kwa ajili ya kusafirisha mizigo.

Tangu kuzinduliwa kwa njia za treni za umeme kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma Juni mwaka jana hadi sasa shirika hilo limesafirisha abiria zaidi ya milioni 1.4.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles