26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

KABWILI AMEFUNGA FAILI LA KAKOLANYA?

Na ZAINAB IDDY

NI zaidi ya miezi miwili sasa tangu mlinda mlango namba moja wa Yanga, Beno Kakolanya, kuamua  kuweka mgomo wa kutoitumikia timu hiyo  kutokana na  kile alichodai kuushinikiza uongozi kumlipa stahiki zake.

Mgomo wa nyanda huyo ulianza wakati Yanga ikijiandaa kusafiri Kanda  ya Ziwa  kuzikabili Mwadui FC na Kagera Sugar.

Ilielezwa Kakolanya alitoroka kambini saa 7 usiku wakati  Yanga ikiwa kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na michezo hiyo. 

Wakati uongozi wa  Yanga ukiwa bado haujatoka na msimamo wake juu ya Kakolanya, kocha mkuu wa timu hiyo,  Mwinyi Zahera, alitangaza  kumwondoa katika kikosi chake na kumtaka kusaka timu nyingine ya kuichezea.

Zahera alisema kitendo cha mlinda mlango huyo kutoroka kambini tena bila kumtaarifu yeye kama kocha, ni utovu wa nidhamu.

Ilielezwa  Kakolanya alikuwa anaidai Yanga kiasi cha Sh milioni 15 ikiwa ni fedha za  usajili.

Lakini kilichomkwaza zaidi Zahera ni hatua ya mdau mmoja wa klabu hiyo kumpa kipa huyo kiasi cha Sh milioni mbili kama sehemu ya  fedha anazodai, ili  arejee kuitumikia timu hiyo.

Hatua hiyo ilimfanya Zahera kufura zaidi akidai kuwa  hatua ya mdai huo inaweza kusababisha migomo zaidi katika kikosi chake, endapo  wachezaji wengine watahisi ni njia sahihi ya kupata haki zao.

Msimamo huo wa Zahera ulisababisha Kakolanya kuiandikia barua Yanga kupitia kwa mwanasheria wake na kuomba mkataba wake kuvunjwa ili awe huru kwenda anakotaka.

Ni ukweli ulio wazi kuwa sakata la Kakolanya kutokuwepo katika kikosi cha Yanga, liliwachanganya mashabiki wa klabu hiyo ambapo baadhi yao walimtupia lawama kocha Zahera kwamba ni tatizo.

Kimsingi sakata hilo liliwagawa mashabiki wa Yanga katika makundi mawili, wanaomuunga mkono Zahera na wanaompinga.

Kundi la waliokuwa wanamuunga mkono Zahera, walidai msimamo wake ulikuwa sahihi kwa vile ulilenga kudumisha nidhamu ya wachezaji.

Wakati wale waliompiga Zahera, waliutaka uongozi kumtimua kocha huyo ili kutoa nafasi kwa Kakolanya kurejea Yanga.

Hawa waliamini  mbadala wa Kakolanya, chipukizi Ramadhan Kabwili asingeweza kumudu  mikikimikiki ya Ligi Kuu hususani mchezo dhidi ya watani wao wa jadi Simba uliochezwa Februari 16, mwaka huu.

Mashabiki waliokuwa upande wa Kakolanya, walienda mbali zaidi na kudai kuwa kipa huyo anahitaji kusamehewa kwa kuwa amekuwa mvumilivu kipindi chote ambacho ameitumikia klabu yao, wakikumbuka  mchezo wao wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Simba ambao aliokoa michomo mingi na kuiwezesha timu yake  iliyozidiwa kila idara kupata suluhu.

Licha ya yote hayo, upepo ni kama umebadilika tena, swali linalosubiri majibu ni nani bado anamkumbuka Kakolanya, nani anahitaji uwepo wake katika kikosi cha Yanga na vipi kama angekuwepo langoni, matokeo inayoyapata Yanga kwa sasa yangekuwa bora zaidi au yangekuwa ovyo?

Hata hivyo, picha inayoonekana, kipa huyo ni kama amesahaulika ghafla, kwani Kabwili ameonekana kushika kasi ili kuwasahaulisha.

Kabwili amekuwa akiaminiwa kiasi kwamba amekuwa akimweka benchi kipa mwenzake, Claus Kindoki.

Kabwili aliuzika rasmi ufalme wa  Kakolanya baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Yanga na  Simba Februari 16, mwaka huu pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao Yanga ilipigwa  bao 1-0, Kabwili alifanikiwa kuokoa hatari nyingi.

Udogo wake wa umri, umbile havikumfanya kuogopa mashuti ya hatari ya nyota wa Simba, Emmaunuel Okwi na John Bocco, badala yake alionekana kuwa kikwazo mbele yao.

Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika, Kabwili alionekana shujaa kwani umahiri wake wa kupangua mipira ya adhabu, vichwa na mashuti ya mbali yaliyokuwa yanapigwa na washambuliaji wa Simba, yalidhihirisha si kipa wa kubahatisha.

Licha ya kupoteza mchezo, hakuna shabiki wa Yanga aliyenyanyua kinywa chake kumtupia lawama Kabwili, badala yake bao lililofungwa timu yao lilionekana la kimchezo.

Kwa mazingira haya, ni wazi hakuna tena matarajio ya kumuona Kakolanya siku za karibuni akirejea kukichezea kikosi hicho cha Jangwani na hili  ni kutokana na uwezo mkubwa wa kinda  Kambwili ambaye anazidi kuimarika siku baada ya siku.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles