KINSHASA, DRC
RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jospeh Kabila amesisitiza kuwa uchaguzi nchini hapa utafanyika Desemba 23 mwkaa huu na kwamba hilo haliwezi kubadilika.
Kabila alikuwa akishutumu vikali muingilio wowote katika mchakato huo wa uchaguzi kutoka mataifa ya kigeni.
Akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani juzi, Rais Kabila amesema kila kitu kitatekelezwa kuhakisha chaguzi zinaendeshwa kwa amani, na haki.
Kabila ameonya kuwa Umoja wa Mataifa hakitakuwa chombo kinachowajumuisha wote iwapo mataifa ya kigeni yataendeleza uingiliaji kati masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Aidha ametaka kuanza mchakato madhubuti wa kuondoka kwa kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Congo (MONUSCO).
Rais huyo wa Congo aliyeingia madarakani mwaka 2001, kisheria haruhusiwi kuwania muhula mwingine baada ya kukamilika kwa muhula wake Desemba 2016.