24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kabendera, akina Kaburu wamwandikia DPP kujadiliana namna ya kumaliza kesi zao

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWANDISHI wa Habari Erick Kabendera,  aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Kaburu, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, wameanza majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya namna ya kumaliza kesi zao.

Hayo yalibainishwa jana mahakamani hapo kwa nyakati tofauti mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile ambapo Wakili Jebra Kambole alieleza kwa niaba ya Kabendera.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Baada ya Wankyo kueleza hayo, Wakili wa utetezi Kambole aliijulisha Mahakama taarifa ya mteja wake kuandika barua  kwa mujibu wa kifungu namba 194A(2) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa mareje mwaka 2019.

Akijibu Wakili Wankyo alidai ni kweli jambo hilo limefanyika na kwamba  Kabendera ameandika barua na ipo katika mchakato na watakapokuwa wamekamilisha wataitaarifu Mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Rwizile aliahirisha Kesi hiyo hadi Oktoba 24, kwa ajili ya kutajwa. Na kama kutakuwa na chochote kabla ya tarehe Jamhuri wataiarifu Mahakama.

Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la utakatishaji wa zaidi ya Sh milioni 173.

Katika shtaka la kwanza ilidaiwa katika kipindi hicho, Kabendera alijihusisha  na mtandao wa kihalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Shtaka la pili ilidaiwa katika kipindi hicho, bila ya sababu, alikwepa kodi ya Sh. 173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu, kabendera anadaiwa kutakaisha Sh 173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kujihusisha na genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

Aveva

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Kaburu  wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Alidai wameshaanza majadiliano ya namna ya kuimaliza kesi hiyo.

Wankyo alidai washtakiwa wote wapo na kesi ilipangwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusiana na hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka kuhusu kusudio la kukata rufaa kupinga mahakama kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji.

Hakimu Simba alisema bado hajamaliza kuandaa hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 18, ambapo atatoa uamuzi huo.

Katika kesi hiyo, wakati mahakama ikitoa uamuzi kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la, iliwaondolea mashtaka mawili ya utakatishaji,  kati ya 10 yaliyokuwa yakiwakabili  Aveva na  Nyange Kaburu baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo.

Hata hivyo, washtakiwa hao pamoja na mwenzao Zacharias Hansppope walikutwa na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa

Kufuatia kuondolewa kwa shtaka hayo ya utakatishaji,  washtakiwa wamepatiwa masharti ya dhamana kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliwanyima dhamana hayapo.

Katika shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Katika shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha dola za Marekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Katika shtaka la tatu Aveva na Kaburu  wanadaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Shtaka la nne Aveva anadaiwa katika banki ya CRDB alitoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa USD 300,000

Aveva anadaiwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia USD 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.

Aveva, Kaburu na Hans Poppe  wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya USD 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577

Shtaka la tisa, Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles