Kabendera aieleza mahakama alivyopatiwa matibabu Amana

0
2146
Mwandishi wa habari, Eric Kabendera, akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kitusu, Dar es Salaam jana kuendelea na kesi yake ya uhujumu uchumi.

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWANDISHI wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba amepatiwa matibabu Hospitali ya Amana baada ya Gereza la Segerea kumpeleka huko juzi.

Hayo yalibainika jana wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai upelelezi haujakamilika, kawasiliana na wapelelezi ambao walidai kuna maeneo muhimu wanayafanyia upelelezi hivyo aliomba kesi iahirishwe.

Wakili wa utetezi Jebra Kambole, alidai wamepokea taarifa hiyo kama ina ukweli na akaikumbusha mahakama kuwa jana ilikuwa imsikilize mshtakiwa kuhusu matibabu aliyopata.

Hakimu Rwizile alimruhusu mshtakiwa kuielezea mahakama.

“Mheshimiwa napenda kuitaarifu mahakama kwamba jana (juzi) nilipelekwa Hospitali ya Amana, nikafanyiwa X ray mgongo, majibu yakatoka kwamba nina matatizo katika pingili.

“Nilichukuliwa vipimo vingine vya damu ambapo majibu yake yatatoka mwishoni mwa wiki, jambo kubwa lilikuwa kupata matibabu ambayo tayari nimeanza kupata,” alisema.

Mahakama baada ya kumsikiliza iliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba mosi kwa kutajwa.

Kabendera anadai bado ana maumivu makali mguu wa kulia na maumivu makali katika mfupa ndani ya paja.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza ni kwamba kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani, anadaiwa alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Inadaiwa shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa kukwepa kodi. Inadaiwa kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, bila sababu za msingi alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, inadaiwa katika tarehe hizo, mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here