26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ wakabidhiwa hospitali ya Sh bilioni 5.6

Na ELIYA MBONEA

ARUSHA

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekabidhiwa rasmi Hospitali ya Jeshi –Arusha yenye thamani ya Sh bilioni 5.6.

Hospitali hiyo ikiwa na vifaa vya kisasa, imejengwa eneo la Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA), Monduli mkoani Arusha, ambapo itachukua wagonjwa 50 wa kulazwa na 300 wa nje.

Akizungumza wilayani hapa juzi wakati wa uzinduzi na makabidhiano ya hospitali hiyo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Alisema kwamba, kuanza kutumika kwa hospitali hiyo kutasaidia askari pamoja na wananchi kupata huduma za matibabu kwa ukaribu zaidi, hususan waliopo jirani.

“Familia za wanajeshi na wananchi wanaozunguka maeneo haya, watanufaika zaidi na ufadhili huu, kwani hii ni hospitali ya kisasa kabisa yenye vifaa vipya na huduma zote zitakuwa zikitolewa.

“Tunaendelea kuwashukuru Ujerumani kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili waweze kutumia vifaa hivi vya kisasa. Lakini pia wafadhili hawa wametujengea chuo cha tiba kilichopo Dar es Salaam,” alisema Dk. Mwinyi.

Alisema kwamba, matumizi ya hospitali za jeshi kwa wastani yamekuwa yakitumiwa kwa asilimia 20 huku asilimia 80 yakitumiwa na wananchi.

“Hivyo basi, kutumika kwa hospitali hiyo, kutakuwa msaada mkubwa zaidi kwa wananchi kwani waliokuwa wakisafiri kwenda hospitali za rufaa, wameletewa huduma hizo karibu.

“Pamoja na hayo, Serikali tutaendelea kushirikiana na wananchi katika huduma zinazotolewa ndani ya jeshi, ikiwamo masuala ya afya na mengine,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter, aliyekabidhi majengo ya hospitali hiyo na vifaa vyake, alisema Serikali ya nchi yake itaendelea kusaidiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali.

Alisema kwamba, miundombinu ya hospitali hiyo iligharimu Sh bilioni 2.8, huku vifaa tiba vikigharimu Sh bilioni 2.8, kwamba fedha hizo zilitolewa na German Armed Force Technical Advisory Group (GAFTAG).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles