Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekibeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ikidai kuwa uchaguzi wa viongozi wake wa juu umewaachia vidonda, majereha na makovu yasiyoisha, hivyo haina shaka kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Hivi karibuni, CHADEMA ilifanya uchaguzi wake wa ndani ambapo Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, akimshinda Freeman Mbowe, ambaye amekiongoza chama hicho kwa zaidi ya miaka 20.
Akizungumza leo Januari 30, 2025, jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Fadhili Maganya, pamoja na Katibu Mkuu wake, Ally Hapi, wamesema CCM tayari imepata wagombea wake na inaendelea kujiandaa na uchaguzi, tofauti na CHADEMA ambayo bado inatibu majeraha ya uchaguzi wake wa ndani.
“Tayari tumepata mgombea wetu, tumejiandaa na uchaguzi. Wao wamemaliza uchaguzi na sasa wanatibu vidonda na majereha. Hakuna sehemu imetulia kama CCM kwa sasa,” amesema Maganya.
Katika hatua nyingine, Maganya ametangaza kuwa Jumuiya ya Wazazi itaandaa kongamano maalumu Februari 2, 2025, kuelekea sherehe za miaka 48 ya CCM, zitakazofanyika Februari 5 jijini Dodoma.
Amesema kongamano hilo litashirikisha wadau mbalimbali, ambapo mada muhimu zitajadiliwa, zikiwemo mchango wa CCM katika maendeleo ya taifa, nafasi ya Dk. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa chama, na umuhimu wa vijana na elimu katika maendeleo.
Maganya amesisitiza kuwa kuelekea miaka 48 ya CCM, chama hicho kina kila sababu ya kujivunia mafanikio yake, ikiwemo amani na maendeleo yanayoonekana nchini.