Nairobi, Kenya
TAKRIBAN watu 15 hawajulikani waliko baada ya jengo la ghorofa saba kuporomoka usiku wa kuamkia jana katika kitongoji cha Kware, Nairobi, Kenya Gazeti la Star liliripoti kuwa watu kadhaa waliokolewa kabla ya jengo hilo kuporomoka.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hilo kuwa jengo hilo lilikuwa limeonyesha dalili ya kuporomoka baada ya kuta zake kuonyesha nyufa.
Mratibu wa uokoaji, Pius Masai alisema zaidi ya watu 100 waliokolewa   na kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Idara inayoshughulikia majanga nchini humo ilisema familia nyingi ziliondoka wakati ziliamriwa kabla ya jengo hilo halijaporomoka na watu 121 walitoka salama.
Vyombo vya habari vinasema baadhi ya watu walirudi ndani ya jengo hilo kuchukua mali zao wakati linaporomoka.
Polisi wanasema hawafahamu ni watu wangapi waliokuwa wamekwama ndani ya jengo hilo lililopomoka.
Aprili mwaka huu watu 49 walifariki dunia wakati jengo lilipoporomoka kutokana na mvua kubwa.