Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema haliridhishwi na mwenendo wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kwa kile walichodai kuwa amekuwa hatoi ushirikiano.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 7,2024 na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, wakati wa mkutano mkuu wa nane wa jukwaa hilo unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema tangu waziri huyo ateuliwe katika wizara hiyo ameshaalikwa mara nne kwenye shughuli za wadau wa habari ukiwemo mkutano huo ambao alipaswa kuwa mgeni rasmi lakini hajawahi kuhudhuria.
“Mwenendo huu hautufurahishi, hatusemi anatujaribu lakini akitaka huo mkondo sisi tuko tayari…ajue moja ya jimbo lake ni vyombo vya habari,” amesema Balile.
Amesema wana ushirikiano mzuri na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo imeanzisha utaratibu wa mashirika na taasisi kukutana na wahariri hatua ambayo imeongeza kiwango cha kuaminiana kati yao.
Jukwaa hilo limesema pia linafarijika kuona juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya habari ambazo zinaipa tasnia hiyo mwelekeo mzuri.
Balile amesema Rais Samia alitoa maelekezo ya kufunguliwa vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na kuagiza kutotumia ubabe kuvidhibiti.
Amesema juhudi hizo zimewezesha Tanzania kupanda katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari kutoka nafasi ya 143 mwaka jana hadi nafasi ya 97 mwaka huu.
“Tanzania ilishuka hadi nafasi ya 143 kwenye uhuru wa vyombo vya habari lakini sasa imepanda hadi nafasi ya 97, hii ni kutokana na uamuzi thabiti na usimamizi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitoa maelekezo mahususi ya kufunguliwa kwa vyombo vya habari,” amesema Balile.
Mwenyekiti huyo wa TEF pia ameiomba Serikali kuendelea kuifanyia maboresho Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ikiwemo takwa la kisheria linalozuia wawekezaji kutoka nje kumiliki zaidi ya asilimia 49 ya hisa.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa ambaye alimwakilisha Waziri Silaa, amesema wanaendelea kupitia sera na sheria mbalimbali kuhakikisha tasnia ya habari inaendelea kuimarika.
Amevitaka vyombo vya habari kuzingatia weledi, maadili, sheria na miongozo inayosimamia sekta hiyo ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.