25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Juhudi zaidi zinahitajika kuzuia mimba za utotoni

WIKI hii, Taasisi ya Msichana Initiative imeiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka sheria za kupinga ndoa za utotoni, ukeketaji na ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike, ili kumsaidia kupata elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, alikaririwa akisema kabla ya utafiti wa mwaka 2015/16 ndoa za utotoni zilikuwa asilimia 37, kwa hiyo kwa utafiti unaosubiriwa kwa sasa ambao unaitwa ‘utafiti wa watu na afya’, ndoa za utotoni zitakuwa zimepungua sana.

Alisema mikoa minne inayoongoza kwa ndoa za utotoni kwa kutumia takwimu za Serikali ni Shinyanga ukiwa na asilimia 59, Tabora, Mara pamoja na Dodoma.

Pamoja na umuhimu wa kujadili changamoto mbalimbali ambazo wasichana wamekuwa wakikutana nazo kwa sababu tu ya jinsia yao, ubaguzi, ukatili wa kijinsia hasahasa ndoa za utotoni pamoja na mazingira hatarishi ambayo wasichana wanakumbana nayo kwenye kufikia ndoto zao, bado tatizo linaonekana kuwepo katika jamii nyingi za Kitanzania.

Gyumi anasema Msichana Initiative, katika kusherehekea siku ya mtoto wa kike duniani chini ya ufadhili wa UN Women wameamua kuandaa mkutano ili kuwakutanisha wadau wanaotetea haki za wasichana kutoka mikoa mbalimbali Tanzania.

Lakini lengo ni kusherehekea kwa  kaulimbiu inayosema “Ndoa za Utotoni: Nguvu za Pamoja Katika Kuchochea Mabadiliko Ya Sheria”.

Hii inajumuisha kuwakutanisha wadau kutoka katika asasi za kiraia, taasisi za kidini, mashirika ya kutetea haki za wanawake, wanaharakati vijana, vyombo vya habari pamoja na wasichana wenyewe.

Lengo la kuwakutanisha wadau hawa ni kujenga nguvu za pamoja kwenye kupinga na kutoa elimu kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na kueleza umuhimu wa kutoa elimu kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na kupinga mabadiliko ya sheria ya ndoa.

Madhara ya ndoa za utotoni yamekuwa yakiainishwa na tayari wamekuwa wakipigania mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 na 17 kinachoruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya mahakama huku mwenye umri wa miaka 15 kufunga ndoa kwa ridhaa ya wazazi.

Ikumbukwe kwamba jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha kuwa umri wa kuolewa unabadilika na kuwa miaka 18 kwa wasichana.

Jitihada hizi ni pamoja na shauri lililopelekwa mahakamani na Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu vipengele hivi vya sheria ya ndoa.

Aidha Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kuwa vipengele hivyo sio vya kikatiba na hivyo sheria ibadilishwe, ingawaje Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mwanasheria Mkuu wa serikali, ilikata rufaa kupinga uamuzi huo wa mahakama.

Pia Oktoba mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ilitoa uamuzi wa mwisho kwamba vipengele hivyo sio vya kikatiba na hivyo iliitaka Serikali kupitia Bunge kuvibadilisha ndani ya mwaka mmoja.

Uamuzi huu ambao ulitolewa na Mahakama ya Rufaa, unatoa wajibu kwa Serikali kuona haja ya ya kuwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake.

Tunatoa wito kwa Serikali kukubali ukweli huu na kujiunga katika juhudi hii, kwa kuhakikisha kuwa sasa inatekeleza wajibu wake na kusimamia mabadiliko hayo ya sheria ili kuongeza nguvu katika kuchochea haki za wasichana nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles