23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JUHUDI ZAHITAJIKA KUIMARISHA MPIRA WA KIKAPU

MPIRA wa kikapu ni miongoni mwa michezo inayofanya vema na kukua kwa kasi hapa nyumbani, tukiachilia mbali soka na riadha.

Licha ya kuwa hadi sasa mchezo wa riadha umeendelea kubeba kumbukumbu ya kufanya vema miaka ya 1970, vipaji vipya vya mchezo huo vimeanza kuonyesha tumaini jipya la kufufua rekodi upya.

Baadhi ya wanariadha wanaoonyesha mwelekeo mwema wa kufufua rekodi hiyo ya mchezo wa riadha ni Alphonce Simbu ambaye hivi karibuni alifanya vizuri katika mashindano ya London Marathon.

Wanariadha wengine ni Sarah Ramadhani, Magdalena Shauri, Saidi Makula na Ezekiel Ngimba ambao kwa pamoja wamepata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano makubwa ya kimataifa.

MTANZANIA tunatambua kuwa upande mwingine  yapo mafanikio yanayokuja kwa kasi yakihusisha mchezo unaozidi kujikusanyia mashabiki; mchezo wa mpira wa kikapu.

Hatua moja inayoonyesha jinsi mchezo huo unavyozidi kufanya vizruri ni hatua ya Shirikisho la Mchezo huo Duniani (FIBA) kutoa mwongozo utakaosaidia vyama wanachama wake kufanya usajili wa klabu pamoja na wachezaji wake.

Katika hatua hiyo, wachezaji sasa hawatasajiliwa kiholela holela katika klabu mbalimbali, bali watatakiwa kuwa na mkataba wa mwaka mmoja ambao utatambuliwa kisheria.

Aidha, klabu zitakazosajiliwa zitatakiwa kuwa na viwanja vyao na mazoezi pamoja na vifaa, kama vigezo vya kusajiliwa na kuendelea kushiriki michuano inayotambulika.

Hii ni nafasi adhimu itakayosababisha kuwepo na nidhamu katika mchezo huu ambao hapo awali haikuwepo.

Nidhamu ni chanzo cha kuchochea maendeleo ya michezo mbalimbali, hivyo hata viongozi wa mchezo huu watakapoamua kuliwekea mkazo suala hili, lazima Tanzania itamiliki wachezaji wazuri wanaoweza kuliwakilisha Taifa vema kwa kuchezea timu  tofauti ulimwenguni kote.

MTANZANIA tumefarijika na hatua hiyo inayolenga maendeleo, ambapo pia tunavishauri vyama vyenye nguvu kama vile Chama cha Mchezo huo jijini Dar es Salaam (BD) chini ya mwenyekiti wake, Okare Emasu, kuanza kujiandaa kufuata utaratibu huo mpya.

Mabadiliko haya kwetu sisi tunayaona ni hatua nzuri, kwani yatasaidia kubadili hali ya mchezo huo na kujenga matumaini mapya kwa wachezaji.

Inakumbukwa awali wachezaji wengi walikuwa wakijitokeza kushiriki mchezo huu kama moja ya kiburudisho na mazoezi, lakini sasa watajiwekea malengo na kuhakikisha wanatimiza ndoto  na matamanio yao ya muda mrefu.

Tunaamini endapo utaratibu huo utaanza kutumika, haitachukua muda mrefu kupata wachezaji watakaoweza kucheza katika ligi maarufu duniani na Watanzania kuonja matunda ya mafanikio katika mchezo huo.

Hivi sasa Tanzania inaendelea kumtupia jicho Hashim Thabeet ambaye anakipiga katika timu ya  Mighty Sport nchini Marekani.

Muda mrefu umepita tangu Mtanzania huyu apate nafasi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania kupitia mchezo wa kikapu, hivyo sasa zinahitajika nguvu mpya ili kuhakikisha nchini yetu inaendelea kushamiri na kung’aa kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles