Mwandishi Wetu- Chato
RAIS Dk. John Magufuli, amewatumia salamu za sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya,huku akiwasisitiza kudumisha umoja,amani na mshikamano
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, baada ya kuungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Chato mkoani Geita aliposali dominika ya 4 ya majilio.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kutoa Chato, ilisema Rais Magufuli alisema wakati Watanzania wanapoelekea msimu wa sikukuu,wakristo na waumini wa madhehebu mengine mbalimbali wanalojukumu la kuendelea kuombea amani, upendo na umoja kwa wanadamu wote bila kubaguana.
“Niwaombe ndugu zangu wa Chato na Watanzania kwa ujumla, tusherehekee sikukuu ya Krismasi kwa amani na upendo mkubwa, tuukaribishe mwaka mpya kwa amani na upendo mkubwa wa Kristo, mwaka unaokuja uwe wa mafanikio, uwe mwaka wa maendeleo, uwe mwaka wa kujenga umoja wetu kwa Watanzania wote, uwe mwaka wa amani na upendo na uwe mwaka wa kuendeleza Taifa letu katika maendeleo ya kweli,”alisema
Rais Magufuli aliwapongeza waumini wa parokia hiyo kwa kazi kubwa ya upanuzi wa kanisa unaoendelea ambayo naye alichangia upanuzi wake mwaka 2016.
Misa takatifu hiyo, iliongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Henry Mulinganisa.