JPM: SITOVUMILIA MAFISADI

0
590
Rais Dk. John Magufuli, akisalimia wananchi baada ya kuwasili jijini Mwanza kwa ziara ya siku mbili jana. Picha na Ikulu
Rais Dk. John Magufuli, akisalimia wananchi baada ya kuwasili jijini Mwanza kwa ziara ya siku mbili jana. Picha na Ikulu

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA

RAIS Dk. John Magufuli, ameahidi kupambana na ufisadi hadi tone la mwisho.

Pamoja na hayo, amesema atahakikisha mfumo wa kipato cha Watanzania una kuwa sawa tofauti na hali ilivyo sasa.

Rais Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jijini Mwanza jana, wakati alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi waliozuia msafara wake, eneo la mzunguko wa Barabara ya Kenyatta, alipokuwa akielekea Ikulu ndogo ya Kapripointi, jijini hapa.

Katika mazungumzo yake, alisema atahakikisha mafisadi waliokuwa wanaishi kwa  kudhulumu mali za wanyonge na kulihujumu Taifa, wanashughulikiwa ipasavyo na vyombo vya kisheria ili nao waweze kuhisi maumivu kama waliyokuwa wanayapata maskini.

“Nashukuru kwa mapokezi makubwa hapa Mwanza kwa sababu tangu natoka uwanja wa ndege, nimeshuhudia mamia ya wananchi pembeni mwa barabara hadi hapa. Hii inaonyesha upendo wenu na naomba niwahakikishie, kwamba Serikali yangu itawafanyia kazi ipasavyo hasa wale mafisadi waliokuwa wakiwanyonya na kuwadhulum mali zenu.

“Nimeamua kupambana na mafisadi hadi tone la mwisho hasa hasa kwenye sekta ya madini kwa sababu nataka kutengeneza maisha ya Watanzania wanaolingana kipato.

“Yaani nataka kusiwe na kundi jingine liko juu sana kuliko wengine, nataka wote tuwe sawa kwani tumeibiwa vya kutosha na sasa nataka niwanyoshe mafisadi mpaka mwenyewe niseme basi.

“Nimefurahi kuona barabara kutoka uwanja wa ndege inajengwa na tunapita bila foleni. Nilipoamua kufuta baadhi za sikukuu zikiwamo muungano, nilijua kuna fedha zilikuwa zinaliwa  na viongozi kadhaa ndiyo maana niliamua fedha hizo zijenge barabara itakayoendelea kuwapo,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Wakati akiendelea kuzungumza, wananchi walilipuka kwa shangwe baada ya kuzungumzia suala la wamachinga ambapo alirudia kwa kuagiza uongozi wa Jiji la Mwanza, usiwasumbue wafanyabiashara hao.

Alisema kwamba, tayari Serikali imeshapata suluhisho la wamachinga hao kwa kuwaandalia vitambulisho vyao ambavyo vitawafanya watambulike na kulipa kodi inayofanana.

Rais Dk. Magufuli aliwasili jijini Mwanza saa 10 jioni na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi wengine wa Serikali.

Leo, atakuwa wilayani Sengerema ambapo pamoja na shughuli zingine, atatembelea mradi wa maji na usafi wa mazingira Sengerema uliopo eneo la Nyamazugo na kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here