JPM: SITABADILIKA

0
605

JPMSITABADILIKA

ELIZABETH HOMBO NA MAULI MUYENJWA

RAIS Dk. John Magufuli amesema kamwe hatabadilika na msimamo wake uko pale pale, na kwamba watu ambao wamekuwa wakilalamika ni wale waliokuwa wakinufaika kula jasho la wengine.

Amesema kuwa anafahamu wapo wanasiasa wachache ambao ‘Mzee Bure’ hajatoka vichwani mwao, wakitegemea kila kitu kifanywe na Serikali.

Kutokana na hilo, amerudia kusisitiza kauli yake kuwa Serikali haina mpango wa kupeleka chakula bure kwa wananchi kwa sababu si jukumu lake.

Pia amesema mtu pekee anayejua kuna njaa ni yeye na kwamba wanaotangaza kuwa kuna njaa ni wale wanaolipwa fedha na wafanyabiashara.

Kauli ya Rais Magufuli, inakuja ikiwa ni siku chache tu baada ya vyombo mbalimbali vya habari kuripoti kuwapo tishio la njaa linalowakumba Watanzania kutokana na ukame.

Akizungumza na wananchi mkoani Simiyu wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa huo jana, Rais Magufuli alisema pamoja na ukame uliopo, wakulima wanapaswa wajipange kulima mazao mengine, badala ya mahindi ambayo huhitaji maji mengi.

Pamoja na mambo mengine, alisema jukumu la Serikali ni kutengeneza miundombinu na si kuwaletea wananchi chakula kwa sababu haina shamba.

“Anayejua kuna njaa nchi hii ni rais… mimi ndiye ninayejua wapi kuna njaa na wapi hakuna. Tanzania hii haina njaa wala watu hawana njaa.

“Nasema sileti chakula, kazi yetu ni kutengeneza mazingira watu waweze kujikimu, hata maandiko matakatifu yanasema asiyefanya kazi na asile na asipokula si atakufa… ninaposema sileti chakula, kweli sileti. Lazima tuseme ukweli.

“Pasiwepo na watu wachache ambao wanataka kufaidi jasho la wengine, tuna kila kitu, ni kwanini tuwe masikini, kuna watu ambao wanachangia tuwe hivyo na ndiyo ninaopambana nao.

“Wakulima na Watanzania kwa ujumla tujipange, tumezoea kulima mahindi wakati yanahitaji maji mengi, tulime mtama, ulezi, viazi, matikitiki maji na mpunga huo ndiyo wito wangu.

“Ninafahamu wako wanasiasa wachache ambao ‘Mzee Bure’ hajatoka vichwani mwao, kila kitu wanataka kifanywe na Serikali,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hakuna njaa, bali kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanatumia magazeti wanayoyaamini kuzungumza Tanzania kuna njaa, lakini lengo lao wameleta mahindi yenye ubora mbovu kutoka Brazil wanataka wasamehewe kodi wayauze Tanzania ikose kodi.

“Yupo mmoja ana tani 25,000 Dar es Salaam nimemwambia tunazikata kodi kama kawaida, nataka niwaeleze huo ndio mchezo wao,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hatapeleka chakula Simiyu na Bariadi kwa sababu ya ukame, na kwamba jukumu la wananchi ni kujua kama mvua ndogo wanapaswa kulima mazao yanayostahimili ukame.

Alisisitiza Watanzania wafanye kazi na kwamba hakuna kugawiwa chakula bure.

“Siwezi kuwasomeshea watoto bure, nijenge barabara, ninunue ndege, nijenge hospitali na kuweka madawa katika hospitali, nilete huduma ya maji na bado watu wakae tu na kusubiri eti Serikali itawatafutia chakula. Watu wafanye kazi ili wapate chakula na si kusubiri chakula cha Serikali.

“Serikali yangu haitatoa chakula… ninaposema sileti chakula sileti kweli wala simung’unyi maneno,” alisisitiza.

Rais alisema kamwe hatabadilika na msimamo wake uko pale pale, na watu ambao wamekuwa wakilalamika ni wale waliokuwa wakinufaika kula jasho la wengine.

Akizungumzia ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Simiyu, alisema ameikataa bajeti iliyokuwa imependekezwa ya Sh bilioni 46 na kuagiza ijengwe kwa gharama ya Sh bilioni 10.

“Haiwezekani jengo hili la ghorofa moja kugharimu kiasi hiki cha fedha… mimi nitaleta Sh bilioni 10, mtu ambaye anaona haiwezekani kujenga kwa fedha hiyo aache kazi… nitakuja kuizindua mwenyewe,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuanzia mwakani, uwanja wa ndege wa Simiyu utaanza kujengwa, ambao utasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo hayo kwa kufanya biashara.

Alimwagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kutangaza tenda kwa wakandarasi ndani ya wiki mbili ili barabara yenye kilomita 48 zilizobaki ianze kutengenezwa.

Aliwataka wananchi wa Simiyu pindi barabara hiyo itakapokamilika waitumie kufanya biashara.

Alisema wale ambao majengo yao yako mita 22.5 kutoka barabarani, waanze kuondoka wenyewe kwa mujibu wa sheria namba saba ya mwaka 2003.

Pamoja na hilo, Rais Magufuli alisema Serikali ina mpango wa kununua meli kubwa nyingine ya kusafirisha abiria itakayokuwapo Ziwa Victoria, baada ya MV Bukoba kuzama.

Pia aliagiza kujengwa kwa tenki la maji yatakayotumiwa na wananchi wa Simiyu kwenye eneo la mlima ambako kulikuwa na mwekezaji, na kwamba akizuia mradi huo afutiwe leseni yake.

“Tenki lijengwe palepale, haiwezekani mtu azuie watu wasipate maji kwa sababu anachimba madini hapo na yeyote atakayekwamisha hilo aache kazi, tena inatakiwa mwekezaji huyo asaidie hata kutujengea watu hawa zaidi ya milioni moja wapate maji,” alisema Rais Magufuli.

 

AMUUMBUA DK. KAMANI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimuumbua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani, ambaye alimwomba aruhusu wafugaji waiingize mifugo katika hifadhi.

Katika hilo, Rais Magufuli alimhoji Dk. Kamani kwamba akiwa Waziri wa Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, kwanini hakufanya hivyo.

“Sasa kama si unafiki ni nini? Mimi si mnafiki, sitaruhusu mifugo kuingia kwenye hifadhi kwa sababu ya sifa za kisiasa huku akiharibu mazingira,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Watanzania waliozoea kuambiwa maneno matamu matamu na wanasiasa huku kukiwa hakuna maendeleo wasahau maneno hayo.

“Nataka Watanzania wasahu maneno matamu matamu… nitaongea ukweli tu, tena ukweli mchungu hata kama utawaudhi, kama ni jiwe nitasema jiwe na si mchanga mgumu uliokusanyika pamoja,” alisema.

Aliwataka Watanzania kuzidi kumwombea kwa sababu wapo wapinzani wake ambao wamekuwa wakimsimanga kwa kununua ndege, na kwamba hao hao wamekuwa wa kwanza kukimbilia kuzipanda ndege hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here