25.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 31, 2023

Contact us: [email protected]

JPM, Ramaphosa wazungumzia fursa za kibiashara

RAIS Dk. John Magufuli amemwomba Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kuwahamasisha zaidi wafanyabiashara wa nchi yake kuja kuwekeza nchini.

Alimwambia kuwa Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuongeza ushirikiano wake na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Ramaphosa.

Rais huyo wa Afrika Kusini aliwasili nchini juzi jioni kwa ziara ya siku tatu na baadaye kuhudhuria mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wamachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) unaofanyika Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo yaliyotanguliwa na mapokezi rasmi yaliyofanyika katika viwanja vya Ikulu, Rais Magufuli alisema katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo na dira ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, Tanzania inawakaribisha wawekezaji mbalimbali.

Alisema Afrika Kusini imepiga hatua kubwa katika viwanda, hivyo amewaalika wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo dawa na vifaa tiba, kuchakata madini na Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.

Rais Magufuli pia alimwomba Rais Ramaphosa kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa nchi hiyo inapokea watalii zaidi ya milioni 10 kwa mwaka ikilinganishwa na watalii milioni 1.5 wanaoingia Tanzania kwa mwaka.

Alisema katika hilo ametoa wito kwa Afrika Kusini kuongeza safari za treni ya watalii na kwa wawekezaji wake kuja kuwekeza katika hoteli na fukwe nchini.

Kwa upande wa biashara, Rais Magufuli alisema Afrika Kusini ni nchi inayoongoza kwa kufanya biashara na Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Sadc.

Rais Magufuli alisema asilimia 70 ya bidhaa za Tanzania zinazokwenda Sadc huenda Afrika Kusini.

Alisema biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini imeendelea kukua ambapo katika mwaka 2018 ilikuwa na Sh trilioni 2. 687 ikilinganishwa na mwaka 2017 ilipokuwa na Sh trilioni 2. 528.

Rais Magufuli pia alimpongeza Rais Ramaphosa kwa kuja na wafanyabiashara ambao wanajadiliana na wafanyabiashara wa Tanzania juu ya kushirikiana kibiashara, na amemhakikishia kuwa Tanzania itakuwa tayari kuhakikisha ushirikiano huo unafanikiwa.

“Sisi Tanzania tumeamua kuwa tunanunua bidhaa zetu Afrika Kusini badala ya kununua bidhaa hizo huko mbali, na kwa kuanzia, pikipiki za kuongozea misafara ya viongozi tutakazotumia wakati huu wa mkutano wa 39 wa Sadc tumenunua Afrika Kusini,” alisema Rais Magufuli.

Naye Rais Ramaphosa alimshukuru Rais Magufuli kwa kumwalika kufanya ziara nchini na amemhakikishia wananchi Afrika Kusini wanaiona Tanzania ni nyumbani.

Alisema Serikali yake ipo tayari kuuendeleza na kuukuza uhusiano mzuri kati yake na Tanzania.

Alieleza kufurahishwa na kuwepo kwa kampuni 228 za Afrika Kusini zilizowekeza nchini na kuajiri zaidi ya watu 21,000.

Aliahidi kwenda kuwahimiza zaidi wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kuja kuwekeza nchini huku akiwakaribisha wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza Afrika Kusini.

Aliipongeza Tanzania kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula na ameahidi kuwa Afrika Kusini itaendelea kununua mazao kutoka Tanzania.

Aidha, Rais Ramaphosa alisema Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika nyanja nyingine mbalimbali zikiwemo afya, ulinzi, usalama na utalii.

Alisema pia amekubaliana na mapendekezo ya Tanzania juu ya mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini hasa wakati huu ambao Sadc inatarajia kuifanya kuwa lugha rasmi ya nne.

Katika ziara hii, Rais Ramaphosa ameongozana na mkewe Dk. Tshepo Motsepe ambaye wakati wa mazungumzo rasmi ya marais alikuwa na mazungumzo na mke wa Rais wa Tanzania, Janeth Magufuli.

Jioni pia, Rais Magufuli na mgeni wake walihudhuria mkutano uliokutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,315FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles