27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Nitaigeuza Ikulu jumba la maonyesho

Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. John Magufuli, akihutubia wanachama wa chama hicho wa Mkoa Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. John Magufuli, akihutubia wanachama wa chama hicho wa Mkoa Dar es Salaam jana.

*Awashangaa wanaohoji atakapopata fedha za kuhamia Dodoma

*Asema atayapiga mnada majengo ya wizara yaliyopo karibu na bahari

*Awataka kina mama kuacha kunywa vidonge vya uzazi wa mpango

AZIZA MASOUD NA ELIAS SIMON (TUDARCO), DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hauwezi kusababisha kuuzwa kwa jengo la Ikulu lililopo Dar es Salaam na badala yake litabaki kuwa jumba la maonyesho.

Kauli hiyo aliitoa jana katika ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizopo Lumumba, Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumkaribisha baada ya kuwasili kutoka katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa alipokwenda kujitambulisha.

Rais Magufuli ambaye alikuwa katika ziara baada ya kuchaguliwa Julai 23, mwaka huu kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, alitumia takribani dakika 50 kuzungumza baada ya kuwasili katika ofisi hizo saa tano asubuhi na alisisitiza kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki ya uongozi wake atahakikisha Serikali yote inahamia Dodoma na kwamba taarifa za kuuzwa kwa Ikulu si za kweli kwa kuwa haiwezekani kuuza jengo hilo ambalo ni muhimu kwa Serikali.

“Serikali yangu itaenda Dodoma, nimeshasema tutaibakiza Ikulu, wengine wanasema Ikulu itauzwa huwezi kuuza jengo la heshima lile, hilo litabaki pale la maonyesho, watu tutakuwa tunakuja pale, kwa hiyo kuhamia Dodoma hakuna mjadala ili Dar es Salaam ipumue,” alisema.

Alisisitiza kuwa uamuzi wa kuhamia Dodoma ni mzuri kwa usalama kwa kuwa eneo kubwa la Jiji la Dar es Salaam limejengwa kando kando ya bahari jambo ambalo si zuri na lipo tofauti na miji mingine inayojengwa katikati, pia linapaswa kuwa la biashara na matembezi kama ilivyo mikoa ya Mwanza na Arusha.

Pia alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma alianza kuusikia tangu akiwa shule ya msingi hivyo muda umefika wa kuutekeleza kwa vitendo.

“Ninafahamu wapo wengine wanazungumza kuhamia Dodoma hakuwezekani, eeeeeh mbele ya Magufuli, kwa sababu haiwezekani wala haingii akilini tangu mwaka 1973 uamuzi ulitolewa wa kuhamia Dodoma lakini haujatekelezwa halafu ndani ya Serikali tuendelee kusuasua, mwaka 1973 mimi nilikuwa shule ya msingi.

“Nimesoma shule ya msingi nikamaliza nikaenda sekondari nikamaliza, nikaenda chuo kikuu nikamaliza hadi nimekuwa waziri hadi leo rais hakuna mtu kuhamia Dodoma yaaah, yaah hatuwezi tukajenga Serikali ya michakato, michakato imetosha,” alisema.

Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya watu wanahoji mpango wa kuhamia Dodoma utakwama kutokana na kutokuwa na fedha.

Pia alisema fedha si tatizo kwa kuwa  Serikali imejipanga kugharamia watumishi kama inavyokuwa katika kipindi cha Bunge.

“Wapo wengine wanasema fedha utatoa wapi? Mbona wakati wa Bunge mawaziri wote wanakaa Dodoma, fedha zinatoka wapi? Si wataenda uko bungeni wakakae huko huko moja kwa moja ukimuona waziri anageuza huku unamwambia kazi hamna.

“Bunge linakaa kule na watu zaidi ya 300, mawaziri wote, manaibu na wakati wa bajeti hadi makatibu wakuu na watendaji tunakaa Dodoma  mbona huwa tunakaa, tuliambiwa sisi ni Dar es Salaam tu,” alisema.

Magufuli alisema kama tatizo ni kukaa Dar es Salaam anazifahamu ofisi zote za Dar es Salaam na atafanya uamuzi wa kuziuza ili fedha zipatikane za kuwahamisha watumishi.

“Nazifahamu ofisi zote za mjini,  ukishatoka pale iliyokuwa Kilimanjaro Hotel zamani inayofuata ni Wizara ya Mambo ya Nje, kuna Takwimu na Wizara ya Ardhi mlolongo huo wote umetizama baharini, nitatangaza tenda watu wanaotaka kujenga hoteli watanunua hayo yote halafu nitamuona nani ataendelea kukaa katika ofisi hizo,” alisema.

KUFUFUA VIWANDA

Akiendelea kuzungumza huku akishangiliwa na mamia ya wanachama wa CCM waliokwenda kumpokea huku baadhi wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na wengine wakiwa wameshikilia yenye picha ya Magufuli yaliyokuwa na maneno ‘Chagua Magufuli’ yaliyokuwa yakitumika katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, alisema mkakati wake wa kufufua viwanda upo pale pale hivyo anahitaji watendaji wake kuchapa kazi.

“Sitaki mtu wa kunikwamisha, spidi yangu ni kubwa, spidi yangu ni hatari ndiyo maana tunataka kujenga na reli ya standard gauge,” alisema.

AOMBA UVUMILIVU KWA WANA CCM

Akizungumzia kuhusu nafasi yake ya uenyekiti wa CCM, alisema amepanga kufanya kazi ili kuondoa kero ndani ya chama hicho.

“Tumepanga kujisahihisha CCM kwa sababu nimekulia humu, kilikuwa kimeanza kupoteza dira na hilo nalisema wazi bila unafiki, kilianza kugeuka kuwa chama cha matajiri, mheshimiwa Katibu Mkuu, Kinana, amezungumza hapa,” alisema na kuongeza:

“Alisema ndani ya chama kulikuwa na tatizo kubwa ambalo ni rushwa lililokuwa linachangia watu kushindwa kuchaguliwa katika nafasi za uongozi.

“Ilikuwa mtu masikini ukiomba uongozi ni vigumu kama kuingia katika tundu la sindano, mimi mwenyewe nimeona, nilipoenda kuchukua fomu nilienda peke yangu na dereva watu wakacheka huyu naye rais watu waliniuliza sera zako ni zipi nikasema zipo katika ilani nikachomoka, wakasema Magufuli awakimbia waandishi.”

Rais Magufuli alisema nchi ilifika mahali imekuwa ya malalamiko kwa kuwa kila mtu alikuwa akilalamika.

“Nataka nirudishe heshima ya chama, nawaomba wana CCM wenzangu wakati nafanya kazi ya kurudisha maadili ya chama mnivumilie, ninaomba mnivumilie kwa sababu nataka mahali ninapoamua kunyoosha nitanyooshea hapo hapo nikikukuta hata uwe kigogo wa namna gani utaondoka tu, nataka CCM mpya,” alisema.

Alisema chama kimeundwa na wanachama wa kawaida na kamwe hatakubali watu watakaotaka kupata uongozi kwa fedha bila kuwa na sifa za kuongoza.

Pia alisema uchaguzi wa viongozi watakaogombea ndani ya chama utafanyika bila kujali dini, kabila jinsia bali wataangalia watu wenye uwezo wa kuongoza.

“Kama kutatokea mtu anataka kutumia fedha au rushwa ajue jina lake halitarudi, mimi nimechaguliwa urais sikutumia hata senti tano, najua kuna viongozi wazuri hawana fedha, nimezunguka peke yangu nataka twende na tuhakikishe tunaondoa kero hizo,” alisema.

Magufuli aliendelea kusema kuwa CCM ina rasilimali nyingi lakini zimekuwa zikitumiwa vibaya na viongozi wajanja  hivyo lengo lake ni kuondoa kikundi cha mafisadi kilichopo ndani ya chama hicho.

“Chama kina rasilimali nyingi, hivi Dar es Salaam tuna viwanja vingapi zaidi ya 100, je, fedha zinazopatikana zinakwenda wapi, jengo la UVCCM nimeambiwa kuna baadhi ya viongozi wamegawana vyumba, nataka nijue wanakusanya kiasi gani na fedha zinakwenda wapi, hayo ndiyo nitayachambua kituo kwa kituo hadi kieleweke,” alisema Magufuli.

Pia alisema Umoja wa Wazazi na Umoja wa Wanawake CCM ni moja ya watu walio na vitega uchumi lakini fedha zake hazionekani zinapoenda.

“Kuna viwanja vya CCM wamezungusha maduka kila kibanda naambiwa watu wanalipa shilingi 30,000 lakini zinazotolewa ni shilingi 500,000, tofauti ya fedha hizo zinaenda wapi maana yake walikuwapo watu wanabeba, hao nitalala nao mbele,” alisema.

Rais Magufuli alisema ilifika hatua baadhi ya viongozi wa UWT walikuwa wakienda kuomba msaada wa fedha za uchaguzi kwa watu waliohama chama nyakati za usiku kwa kujificha kutokana na kuwapo kwa matumizi mabovu ya rasilimali.

“Hivi niulize kwanini Redio Uhuru haina fedha, kwanini bendi ya TOT wafanyakazi wake wanakonda, hivi CCM kwanini haina televisheni.

“Sasa nataka chama safi kilichookoka asiyekubali kubadilika tutamlazimisha asipotaka hatutakubembeleza tutakuacha tuendelee na safari, tunataka chama tawala na si cha kubembeleza kutawala,” alisema Magufuli.

Alisema haiwezekani CCM iendelee kuwa chama cha kuomba omba kwa wafanyabiashara kipindi cha uchaguzi wakati rasilimali zilizopo zinaweza kuendesha chama.

Kuhusu yeye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, alisema inawezekana kuna watu wachache hawajafurahi lakini wanapaswa kuvumilia ili uongozi wake uwafaidishe watu wengi.

“Inawezekana sikustahili kupewa uenyekiti CCM, lakini mliamua kwa upendo wenu kwamba tunampa Magufuli  kwa asilimia 100, nimebaki na deni kubwa la kuwatumikia kwanza wa CCM, pili Watanzania wote, nataka niwaahidi kwa upendo mkubwa kwa kumtanguliza Mungu nitatumia akili zangu na nguvu zangu zote kuwafanyia kazi,” alisema.

Akizungumzia elimu, alisema kitendo cha Serikali kutoa elimu bure kimechangia kuongeza udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka milioni moja kwa mwaka jana hadi milioni mbili.

“Hii inaonyesha hawa milioni moja kusingekuwa na elimu bure wangebaki nyumbani, sasa Watanzania kipindi changu elimu ni bure hakuna mtu atakayerudishwa nyumbani wala kulipa hata senti tano, jamani sasa kazi yetu ni kuzaa tu.

“Wanawake wasihangaike hata kunywa vidonge vya majira, wewe fyatua tu mtoto atasoma bure msingi hadi wa sekondari na awe wa CUF, CCM au Ukawa labda baada ya mimi kuondoka madarakani ndiyo mnywe vidonge vya majira,” alisema.

AMSHUKURU KIKWETE

Pia alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwamba ndiye aliyechangia kumfikisha hapo alipo.

Magufuli ametoa kauli hiyo wakati siku za nyuma alipozungumza na wakandarasi alinukuliwa akisema kuwa urais wake umetokana na Mungu.

“Nawashukuru viongozi wote wastaafu, akiwemo Rais mstaafu Kikwete, yeye asingetaka niwe hapa nisingekuwepo,” alisema Magufuli.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alimwahidi Magufuli kuendesha chama hicho kwa kasi aliyonayo na si vinginevyo ili kusaidia Watanzania.

“Najua ulivyo mkali kidogo na unavyojitahidi kuleta kashikashi na mimi nitaenda hivyo ili kuwakomboa wanyonge, nakuhakikishia chini ya uongozi wangu kwa kuwa Watanzania wanakufahamu ulivyo makini na mimi nitajitahidi kwenda na kasi hiyo, nakupongeza upindishi maneno unasema moja kwa moja,” alisema.

Kinana alisema katika kipindi hiki hakuna mtu atakayepata uongozi kwa njia za panya ikiwemo rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles