24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: NITAENDELEA WAKUWANYOFOA WAPINZANI

Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amesema ataendelea kuchukua viongozi wenye akili kutoka vyama vya upinzani na katu hana muda na wanaopiga kelele na vilaza.

Alisema viongozi vilaza katika vyama vya upinzani wamebaki kupiga kelele na kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Kauli hiyo aliitoa   mjini Tabora jana baada ya kuzindua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na upanuzi wa uwanja wa ndege wa mkoa huo.

Alisema lengo lake ni kuhakikisha wale anaowateua kutoka katika vyama vya upinzani wanafanyakazi bila kujali vyama vyao na badala yake wanajituma kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Rais Dk. Magufuli alisema viongozi vilaza wataendelea kubaki na kupiga kelele bila hoja za msingi kwa sababu wananchi wanahitaji maendeleo na wala hawataki kusikia mambo ya ajabu.

“Nitaendelea kuwanyofoa viongozi wa upinzani, wale wenye akili ili waje kuwatumikia wananchi kwa sababu wanataka maendeleo, wale vilaza waache wabaki kupiga kelele, wananchotaka wananchi ni maendeleo tu na siyo maneno yao.

“Kwa sababu maendeleo hayana chama, ukabila, dini wala rangi, yapo kwa ajili ya wananchi.

“Hivyo basi nitahakikisha wananchi wanapata maendeleo kwa kila hali hasa kwa kutumia fedha zetu za ndani,” alisema Dk. Magufuli.

Kauli ya Rais Magufuli kuhusu uteuzi kutoka vyama vya upinzani  ilitanguliwa na ile ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo aliyeteuliwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, kumsifu Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya kwa ajili ya Watanzania wote.

Alisema  mkuu huyo wa nchi amekuwa  akienzi misingi ya nchi  iliyoasisiwa tangu Uhuru ambayo ni umoja, uzalendo sambamba na kupinga ukabila katika kuwatumikia Watanzania.

“Kwanza nikushukuru sana kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii na ninapenda kusema hapa katu sitakuanguasha katika majukumu haya uliyonipa mimi wa chama kingine.

“Kwangu Rais Magufuli amevunja mwiko wa chama chake CCM na hata upinzani kwa kutushirikisha katika Serikali yake,” alisem Prof. Kitila.

Akizungumzia ujenzi wa reli ya kisasa, Rais Dk. Magufuli alisema katika kipindi hiki ambacho serikali inajenga reli ya kisasa ya kutumia umeme, itawasaidia wananchi wa mkoa huo kufanya biashara kwenda nchi mbalimbali zikiwamo za Afrika Mashariki, jambo ambalo linaweza kuinua uchumi na biashara.

Alisema reli iliyopo iliyojengwa na serikali ya Ujerumani mwaka 1905 na kumalizika kipindi cha serikali ya Uingereza mwaka 1919 imekwisha kuchakaa, hivyo  serikali imemalizika kujenga reli ya kisasa kwa ajili ya kuimarisha safari za biashara na uchumi.

“Reli hii ni kongwe imejengwa miaka 100 iliyopita, hivyo   wananchi ndiyo wameifuata, lakini siyo reli imefuata wananchi.

“Wito wangu kwetu, bomoeni nyumba zenu   kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itawasaidia kusafiri kwa kutumia dakika 60,”alisema.

Alisema  lengo la serikali ni kuhakikisha   treni zinazoonekana Ulaya zije Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi na hayo ndiyo maendeleo wanayotaka wananchi.

Akieleza kuhusu mradi wa maji, alisema Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa yenye matatizo ya maji, jambo ambalo limemfanya kufikia  makubaliano na serikali ya India  kutoa msaada wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.

Alisema serikali ya India kupitia kwa Waziri Mkuu wake, imeweza kusaini   Sh bilioni 601 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji.

“Tumesaini makubaliano ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 89 mkoani humu, lengo ni kuhakikisha   wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

“Mradi huu utakamilika katika kipindi cha miaka miwili hadi miwili na nusu,”alisema.

Kiama cha Ma-RC, DC

Akizungumzia   mabango yaliyokuwa yanaonyeshwa na wananchi, Rais Magufuli alisema mabango hayo ni kero zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa mikoa kushindwa kutatua kero za wananchi.

Rais Magufuli alisema kuanzia sasa ataanza kufanya ziara  nchi nzima   kubaini kero za wananchi ikiwamo kujua wakuu wa mikoa na wilaya walioshindwa kusikiliza kero za wananchi.

Alisema wale ambao watashindwa kufanya hivyo atalala nao mbele kwa sababu  kuwapo mabango kwenye mikutano yake ni kielelezo cha viongozi hao kushindwa kusikiliza kero za wananchi kwa wakati.

“Kuanzia sasa nitafanya ziara mikoani na wakuu wa mikoa na wilaya watakaoshindwa kusikiliza kero za wananchi nitalala nao mbele.

“Maana sasa imefika wakati wananchi ndiyo wanaomba msaada wa viongozi wakubwa wakati wewe niliyekuchagua upo.

“Nimesoma mabango yote, nimemwambia mtendaji wangu ayapige picha halafu nikirudi Dar es Salaam, nitaweka kwenye CD kwa ajili ya kuyasoma.

“Najua mkoa huu unaongoza kwa migogoro ya ardhi kama kuna maofisa ardhi, magereza, watendaji wa halmashauri wanawaponyoka wananchi ardhi zao, nitawatumbua.

“Mimi nakujua Mkuu wa Mkoa ndiyo niliyekukabidhi mkoa huu, kaa na watendaji wako angalia namna ya kutatua kero za wananchi, siyo kusubiri rais aje ndipo wananchi waanze kulalamika.

“Masuala mengine yanapaswa kutatuliwa huku chini,” alisema.

bashe

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa utekelezaji wa ahadi zake za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambazo zimefanikiwa kwa asilimia 80.

Alisema waliahidi ujenzi wa shule za sekondari ya kidato cha tano ambayo ujenzi wake ameuanzisha.

“Mheshimiwa Rais naomba nikueleze, Profesa Ndalichako (Waziri wa Elimu) ametupatia Sh milioni 259.

“Mwishoni mwa mwaka huu tutafungua shule ya kidato cha tano na sita na pia niliomba fedha za maji katika Mji wa Nzega na ulivyopita Desemba niliomba Sh milioni 400.

“Na kwa taarifa nimshukuru Waziri wa Maji Injinia Lwenge na ndugu yangu Kitila Mkumbo, wametupatia Sh milioni 200 za awali.  Nakuomba ukiwa unazungumza nao watumalizie zilizobaki,” alisem Bashe.

Alisema historia ya Taifa ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1961 lakini hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli alianzisha mapambano ya uchumi.

“Ninataka kuwaambia wananchi wa Tabora kuwa ililetwa sheria ya masuala ya madini kama njia ya kulinda rasilimali za nchi. Mheshimiwa Rais usisikilize kelele za watu wasiotoka kwenye maeneo ya migodi hawajui dhuluma waliyopata wananchi ambayo maeneo yao yana dhahabu.

“Mheshimiwa Rais pale Nzega tulikuwa na Kampuni inaitwa Resolute.

“Nataka nikuambie service levy (ushuru wa halmashauri) wamelipa kwa miaka miwili, leo wanaondoka wanadaiwa Sh bilioni 10.

“Na sasa wameleta madai yao ya tax refund za VAT na mafuta wakiitaka Serikali iwarudishie fedha hizo, ninakuomba  mwambie Kamishna Mkuu wa TRA, Waziri wa Fedha wasiwalipe mpaka watoe Sh  bilioni 10 za Halmashauri ya Nzega.

“Miaka mitano ya Kigwangwalla amepigwa mabomu na ninataka nikuambie vita hii ya rasilimali hauko peke yako tuko pamoja na wewe, wametuachia mahandaki.

“Wanasema Magufuli mkali, mimi nimejiuliza hivi huyu mzee ni mkali kweli?  Nimekuja kugundua kumbe ulipita seminari na unafundishwa ukipigwa kulia weka na kushoto.

“Sisi kwenye Uislamu tunaambiwa jino  kwa jino najiuliza umewaambia utawafungia hawa watu, inatakiwa kufungiwa migodi leo.

“Hakuna njia ya kujadiliana na mwizi duniani, kumpa nafasi mwizi.

“Utakapomteua Mtendaji Mkuu  wa Divisheni ya Madini, Katibu Mtendaji, naomba wape jukumu moja waanzishe masoko ya dhahabu katika maeneo ambayo wachimbaji wadogo waliko kwani wana uwezo wa kuzalisha dhahabu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles