29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Ndege za Rais zibebe abiria

AZIZA MASOUD Na AGATHA CHARLES

RAIS Dk. John Magufuli, ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kuzipaka rangi ndege mbili kati ya tatu zinazotumiwa na Rais ili zitumiwe na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kusafirishia abiria.

Kauli hiyo aliitoa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana wakati akipokea ndege mpya ya sita aina ya Airbus A220-300.

Magufuli alisema ndege hizo ambazo ni Fokker 28 na Fokker 50, zilizonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya Rais zinapaswa kuungana na nyingine sita zilizopo kwa ajili ya kusafirisha abiria maeneo mbalimbali.

“Rais mwenyewe kwanza hatembei tembei, kwanini ndege ikae imepakiwa tu. Kwa hiyo ndege ya Fokker 28, Fokker 50 inayobeba watu karibu 50 nazo zitapakwa rangi za Air Tanzania,” alisema Rais.

Pia alisema hatua hiyo ni kuongeza ndege za kutosha ndani ya shirika hilo ili zibebe wananchi pamoja na watalii.

“Mafanikio ya ndege hiyo ya sita ni ushuhuda tosha wa nguvu za Watanzania.

“Ndege hizi ni zenu, hakuna hata senti tano iliyonunua ndege hizi kutoka kwa mfadhili yeyote. Mfadhili ni Watanzania,” alisema.

Alisema ATCL ni shirika linalomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 kutokana na kodi zinazolipwa.

Alisema ni wajibu wa wahusika wanaokusanya kodi kuhakikisha kuwa fedha hizo hazipotei ili zitumike ipasavyo.

“Kwa taarifa yenu, kule kuchelewa tu ndege, kuileta hapa kampuni ya Bombardier imetulipa fedha kiasi cha dola milioni 1.3. Ile nyingine iliyokuja ile ya mbele Dodoma ilichelewa kidogo siku kadhaa, wakawa wanatulipa kila siku dola elfu tano. Hii wameichelewesha kidogo tukasema hakuna cha kuchelewesha, wamelipa tena hizo dola. Ndiyo biashara inavyoenda. Kwa hiyo wameandika cheki ya dola milioni 1.3 wanaipeleka Wizara ya Fedha,” alisema.   

Magufuli alisema hiyo ndiyo Tanzania anayotaka ya ukweli na uwazi kwa sababu walipokuwa Canada aliwaambia waandike hundi na kuja nayo na ndivyo walivyofanya.

Alisema ingekuwa katika miaka mingine fedha hizo zisingerudi kwa sababu angeenda mtu huko na kuzichukua.

Pia alisema nchi itakuwa na marubani 60 wa ndege na waliopo ni 50 hivyo ni fursa kwa Watanzania.

“Kutoka Portugal hadi Abidjan aliyeongoza ndege na kuiendesha kwenye mawingu kule kwa spidi zote ni Mtanzania, ndugu Msingi, kijana mdogo tu, wala hana majivuno. Ameendesha kwa saa tano. Hapo ndipo muanze kujua vijana mnaweza.

“Kutoka Abidjan hadi Dar es Salaam ni yule jamaa mwenye ndevundevu kijana anaitwa Budodi, hakusaidiwa na mtu hadi ametua, hizi ndege zingekuwa hazipo wangeendesha nini, si matoroli kule mjini,” alisema.

Pia alisema ndege hiyo ya sita si ya mwisho, kwa sababu baada ya ile Dream Liner inayobeba watu 262 itakuja nyingine ya aina hiyo ikiwa na uwezo wa kubeba watu 262 na itawasili mwishoni mwa mwaka huu ikitokea nchini Marekani.

“Kwa hiyo Dream Liner zitakuwa mbili, Air Bus zitakuwa mbili, zitapishana katika masafa ndani ya Afrika na nje ya Afrika. Lakini pia tumenunua ndege nyingine Bombardier, ili ziwe nne nayo italetwa mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao. Hivyo tutakuwa na ndege nane,” alisema.

Magufuli alisema ndege ndogo iliyokuwa na matatizo kidogo itafanyiwa ukarabati hivyo kufanya idadi ya ndege kuwa tisa.

Katika hatua nyingine, alisema viongozi wa dini wameanza ukurasa mpya kwa kuwa pamoja hasa katika hafla iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Alisema Askofu Zachary Kakobe, alimweleza kuwa kama ambavyo viongozi wa dini walivyokutana ndivyo na wanasiasa wanapaswa kukutana.

“Mimi nakubali sana, huwezi ukakutana na mtu anakwambia pale uchinjwe chinjwe utupwe baharini. Utaogopa kwamba siku ukikutana naye ndiyo siku ya kuchinjwa kwa hiyo unamwacha anakaa peke yake kule. Mmeanza vizuri nyie watu wa dini ni matumaini, ni mwelekeo mzuri wa kutengeneza Tanzania mpya. Tunajifunza kutoka kwenu. Uvumilivu wenu ni muhimu hata sisi wanasiasa tukawa nao,” alisema.

Magufuli alisema hakuna nchi duniani iliyotoka katika umasikini ikafanikiwa na kuwa tajiri kwa sababu ilipewa msaada na nchi nyingine.

“Ili nchi iendelee ni lazima ijitegemee, ndiyo maana nawaomba Watanzania mlitambue hilo, kwamba dhana ya kujitegemea ndani ya Utanzania ndiyo itakayotuokoa kubadilisha maisha ya Watanzania. Saa nyingine ukipewa misaada sana inakulemaza, iwe ya kukuwezesha kujitegemea zaidi. Ushirikiano na nchi zingine ulenge kumwinua Mtanzania katika maendeleo.”

Alisema wanahitajika wawekezaji kutoka nje lakini ni lazima jumuiya ya wafanyabiashara wa ndani ijengwe ili waweze kuanzisha biashara kubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Pia aliwataka ATCL kuacha kufanya matumizi mabovu kwa kuwa Serikali inahitaji shirika hilo lijiendeshe kwa faida.

“Wito wangu muache matumizi ya ovyo, zamani kuna wakati ndege inaondoka kuchukua vitu vya watu fulani, tunataka baada ya miaka kumi tuwe na ndege hata 100 watu wakuendesha wapo, wapo watu wanalipwa visenti msiwafuatishe.
“Mkurugenzi wa ATCL alikuwa anafanya kazi Senegal na mshahara mkubwa lakini tulipoanzisha shirika tukaamua kumwomba kuja kulisimamia shirika, huo ndio uzalendo, wazalendo Watanzania wapo,” alisema.

Alisema ATCL wanapaswa kufahamu kuwa ndege hizo wamekodishwa hivyo wanaweza kupokonywa wasipoziendesha vizuri.
“ATCL lazima wajue hizi ndege wamekodishwa wakienda ovyo tunawapokonya, naliweka wazi wakifanya kazi ovyo tunaweza tukavunja mkataba tukawapa hata Precision Air tunabadili tu rangi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles