23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Nataka vyama vingi viendelee

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

Rais Dk. John Magufuli amesema tamanio lake ni kuona kunakuwepo vyama vingi vitakavyoleta ushindani, kwa sababu suala hilo lipo kwa mujibu wa katiba na sheria.

Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela katika ziara yake ya siku nane mkoani Mbeya.

“Mkuu wa Mkoa (Albert Chalamila) anatamani kuwa na chama kimoja, mimi natamani vyama vingi sana vitakavyoleta ushindani, lakini siku zote CCM ndicho kilichokuwa kinashinda.

“Kwahiyo kila mmoja ana tamanio lake, mimi tamanio langu ni kuwa na vyama vingi kwa sababu ni kwa mujibu wa katiba na sheria,” alisema Rais Magufuli.

ALIYOSEMA CHALAMILA

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alisema haoni sababu ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini badala yake kuwe na chama kimoja tu kitakachoitwa ‘Magufuli Ruling Party’.

 “Mheshimiwa Rais umefanya mengi sana mema kwa nchi yetu, umetoa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, hapa Kyela umetupatia vitambulisho 10,000, wananchi 8,850 wameshagawiwa vitambulisho hivyo kwa gharama ya Sh 20,000 kwa kila kitambulisho. 

“Katika suala la elimu bure, katika Mkoa wa Mbeya unawalipia wanafunzi wa shule za msingi zaidi ya 400,000 na wa sekondari zaidi ya 86,000.  Tunakushukuru sana.

“Katika mazuri haya unayoyafanya, sioni kama kuna haja ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa, badala yake kuwe na chama kimoja tu kinachoitwa ‘Magufuli Ruling Party’,” alisema Chalamila.

JPM AMFAGILIA MWAKYEMBE

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ni mchapakazi na aliwahi kunyweshwa sumu kwa sababu ya kusimamia haki.

“Mwakyembe alikuwa naibu waziri wangu (Wizara ya Ujenzi), alinisumbua sana na hili nalisema wazi, alinisumbua kweli kweli na amewahi kunyweshwa sumu akapelekwa nje kwa sababu ya kusimamia haki.

“Inawezekana ninyi watu wa Kyela hamumjui vizuri Mwakyembe, sikuja kumpigia kampeni,” alisema.

SHERIA YA KUWALINDA WAKULIMA

Rais Magufuli alipiga marufuku wakurugenzi na watendaji wa halmashauri kuwatoza ushuru wasafirishaji wa mazao chini ya tani moja na wafanyabiashara wadogo wenye vitambulisho vya wajasiriamali.

Alisema wapo watendaji wa halmashauri wanaoendelea kutoza ushuru kwa wafanyabiashara hao kwa kudhani wanapoacha wanapunguza mapato.

“Sasa leo narudia kwa wakurugenzi na watendaji wote wa halmashauri, msiwatoze wananchi ushuru wa mzigo wowote usiozidi tani moja.

“Mkulima wewe safirisha kutoka hapa peleka mahala popote, hakuna wa kukutoza ushuru na hii sheria imepitishwa na Bunge hayupo yeyote wa kuitengua, kwa hivyo mkurugenzi ukitengua umevunja sheria, una wajibu wa kufukuzwa kazi.

“Tuzingatie sheria ya kuwalinda wakulima, pakia viazi, maharage, njugu, chochote ilimradi kisizidi tani moja hakuna kulipia, ukizidisha mie simo,” alisema.

VITAMBULISHO KWA WAFANYABIASHARA WADOGO

Kuhusu vitambulisho vinavyotolewa kwa wafanyabiashara wadogo wenye mtaji chini ya Sh milioni 4, Rais Magufuli alisema hatua ya kuvitoa inawaumiza watendaji kwa kuwa huko nyuma walizoea kula.

“Wapo wanaouza uji, mahindi sokoni, mchicha, maandazi, vitumbua mtaji wake hauwezi kufika Sh milioni 4 kwa mwaka, ukishakuwa na kitambulisho chako unalipia Sh 20,000 kwa mwaka mzima.

“Na utafanya biashara popote mradi hauvunji sheria, hakuna wa kukubughudhi, viongozi na madiwani mtoe ufafanuzi kwa wananchi hawa wafaidike na matunda ya kuwa Watanzania,” alisema Rais Magufuli.      

KAZI USIKU NA MCHANA

Aidha alisema wananchi wanapaswa kutambua Serikali iliyopo madarakani hailali usiku na mchana inafanya kazi kwa faida yao na waangalie walipotoka, walipo na wanapoenda.

 “Unafanya hiki unamaliza unaingia kingine, haiwezekani ukavifanya vyote, unatengeneza barabara yenye gharama ya Sh bilioni 60, barabara unamaliza, huku umeme kila mahali unawaka, elimu bure, huku unaajiri madaktari, walimu, kule unajenga vituo vya afya, ndiyo maana nashindwa hata kunenepa.

“Mwanzoni mwa mwezi huu nikiwa katika ziara mkoani Ruvuma nilizindua vituo vya afya 352. Vituo vya afya Tanzania nzima vimekamilika, havikujengwa na hewa, ni fedha za walipakodi mkiwamo ninyi, fedha hazikutolewa na wafadhili wowote.

“Tungewapelekea wasingetoa, tumejenga kwa gharama zetu. Umeme kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100. Fedha hizo zimepatikana baada ya kuwabana mafisadi na walarushwa.

“Tumewabana mafisadi ndiyo maana tumepata, tusingefanya hivyo tusingefanikiwa. Tumeamua kupambana na walarushwa na hiyo ni kazi ngumu kwa kuwa hawana alama katika uso, unaweza kukuta mwana CCM kumbe ni fisadi, Chadema kumbe fisadi kweli kweli, unaweza kukuta hana chama lakini ni fisadi,” alisema.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imeongeza fedha za dawa kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 270 kwa ajili ya kununua dawa, elimu bure kila mwezi Sh bilioni 23.86  zinatolewa.

“Tunafanya haya kuhakikisha kila mwenye haki anapata haki yake, tumenunua ndege nane kwa mpigo tena mpya watu walipiga vita mno, mara kwanini hatukopi, unayo fedha sasa unakopa ya nini.

“Kwa sasa tunapanua viwanja 11 vya ndege, tunataka maparachichi yabebwe moja kwa moja hadi kwenye masoko, unamkuta mtu mmoja amelewa tikiti maji anaongea vitu havieleweki.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kiwango kikubwa mno, haya yote shetani hajalala, wapo watakaotamka ambayo hata hayatakiwi, wapo watakaoona wivu kwanini yanatokea,” alisema.

JOSEPH KAKUNDA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alisema pamoja na kwamba Kyela inazalisha mazao mengi, ni vyema ikaanzisha viwanda kwa ajili ya kuchakata mazao ili kukuza uchumi.

Alisema wizara yake ikishirikiana na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe wanafanya utaratibu wa kuhakikisha viwanda vinajengwa ili mazao mengi yanayozalishwa yaweze kuongezwa thamani.

“Mazingira ya viwanda na biashara ni makubwa hapa Kyela, wanazalisha mpunga kilo milioni 68 kwanini msiwe na kiwanda kikubwa cha kuchakata mpunga na kupaki mchele kwa ajili ya soko la kimataifa.

“Tutawasaidia kuwaletea viwanda, cocoa inazalishwa tani 8,250 ina maana mnahitaji kiwanda cha kuchakata cocoa hapa mtengeneze chocolate, lazima twende na mazingira yanayohitajika kibiashara, nitamwagiza meneja wa Sido mkoa aweke kambi Kyela ili kusaidia viwanda vidogovidogo,” alisema Kakunda.

JAPHET HASUNGA

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema mazao yanazalishwa kwa wingi eneo hilo na kwamba Kyela ni eneo linalozalisha chakula kwa wingi.

“Wapo watu walikuwa wanatumia eneo hili kwa masilahi binafsi na aliyekuwa analeta shida tulishamwondoa, tutahakikisha pembejeo zinapatikana na wakulima wanaendelea kulima,” alisema Hasunga.

SELEMANI JAFO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo alisema Rais Magufuli ametoa Sh bilioni 284.5 kuboresha na kujenga vituo vipya vya afya nchini.

 “Tukizungumzia sekta ya afya, juzi  tu kule Mbonde Mtwara Rais umezindua kituo cha afya kikiwa ni miongoni mwa vituo vya afya vilivyoboreshwa 352, vituo vya afya vipya 67 ambavyo vimetumia Sh bilioni 284.5,” alisema.

Alisema Rais Magufuli ameidhinisha Sh bilioni 52.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule, madarasa, nyumba za walimu na vyoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles